Wednesday 26 May 2021

Dkt. Bashiru Atema Nyongo Bungeni Kwa Mara ya Kwanza

...


Dr Bashiru Ally, Mbunge wa Kuteuliwa na Rais, jana tarehe 25 Mei 2021, amesimama bungeni kwa mara ya kwanza na kutumia jukwaa hilo kuzungumzia masuala mbalimbali yaliyojitokeza nchini, tangu aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano, Hayati John Magufuli, kufariki dunia.

Magufuli alifariki dunia tarehe 17 Machi 2021, kwa ugonjwa wa moyo, katika Hospitali ya Mzena mkoani Dar es Salaam, kisha mwili wake kuzikwa nyumbani kwao Chato mkoani Geita, tarehe 26 Machi mwaka huu.

Akizungumza bungeni jijini Dodoma, Dk. Bashiru amesema Tanzania ilipitia misukosuko mingi kufuatia kifo cha Magufuli, lakini kwa neema za Mungu, ilivuka salama.

“Kwa kuwa ni mara ya kwanza kuongea, nianze kwa kumshukuru Mungu kwa kutuneemesha na kuivusha nchi yetu, katika kipindi cha misukosuko baada ya kupata msiba mkubwa ambao haujawahi kutokea katika nchi yetu. Ninahakika Mungu hatatutupa,” amesema Dk. Bashiru.

Dk. Bashiru aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi siku za mwisho za uongozi wa Magufuli, amesema baada ya kifo cha kiongozi huyo kutokea, kulitokea majaribio kadhaa yaliyokuwa na lengo la kuitikisa nchi, lakini hayakufanikiwa.

“Yalikuwepo majaribio ya kupitisha maneno na kutuchonganisha, wakati mwingine kudhalilisha watu na kutunga maneno ya uongo, ili nchi itikisike. Lakini nasema wameshindwa na wamelegea,” amesema Dk. Bashiru.

Tarehe 27 Februari mwaka huu, Magufuli alimteua Dk. Bashiru kuwa Katibu Mkuu Kiongozi, baada ya aliyekuwa anashika nafasi hiyo, Balozi John Kijazi, kufariki dunia.

Hata hivyo, mwanasiasa huyo alihudumu kwenye nafasi hiyo kwa muda wa siku 32, baada ya Rais wa Awamu ya Sita, Samia Suluhu Hassan, kumteua kuwa mbunge kisha nafasi hiyo kuikabidhi kwa Balozi Hussein Katanga.

Dk. Bashiru amempongeza Rais Samia, baada ya kuapishwa kuwa Rais wa Tanzania, tarehe 19 Machi 2021, Ikulu jijini Dar es Salaam.

Aidha, Dk. Bashiru amemshukuru Rais Samia kwa kumteua kuwa mbunge, huku akimuahidi kutomuangusha katika kuitumikia nafasi hiyo.


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger