Thursday, 20 May 2021

DIAMOND PLATNUMZ AIKOSOA FORBES ORODHA YA WANAMUZIKI MATAJIRI.... 'YA KIJINGA'

...
Diamond Platnumz amekasirishwa na orodha ya wanamuziki matajiri alioitaja kuwa ‘ya kijinga’.

Mwanamuziki huyo ambaye ni mmoja wa nyota wa muziki Afrika amekosoa orodha hiyo ya Forbes iliyotolewa hivi karibuni ikiwaonesha wanamuziki tajiri wa bara hili na kumuweka katika nafasi ya 20.

‘’Wakati mwengine nitafuteni katika Google ili kujua thamani yangu’’, Diamond aliandika katika mtandao wake wa Instagram ‘’kabla ya kuniweka katika orodha yenu ya matajiri !

Nyota huyo wa muziki nchini Tanzania mwaka uliopita alikuwa mwanamuziki wa kwanza katika jangwa la Sahara kufikisha watazamaji bilioni moja katika mtandao wa YouTube.

Ijapokuwa anapinga thamani yake kuwa $5.1m, yeye mwenyewe hajaitangaza hadharani.

BBC imewasiliana na usimamizi wa Diamond ili kupata tamko.

Siku ya Jumanne msanii huyo ambaye ni namba moja Afrika Mashariki, na Rais wa WCB Wasafi, aliandika historia nyingine tena baada ya kutia saini mkataba na kampuni ya muziki ya Afrika Kusini, Warner Music.

Mkataba huo mpya utahakikisha kuwa WCB Wasafi imejumuishwa katika Warner Music Afrika Kusini na Ziiki Media, wakati mtandao wa Warner Music ukisaidia kumfanya Diamond Platnumz na wasanii wa lebo hiyo kupanda hadhira ya ulimwengu.

Diamond Platnumz ni mmoja wa wasanii waliofaulu zaidi Afrika, akiwa ameachia nyimbo zaidi ya 30, ukurasa wake wa YouTube ukiwa na zaidi ya mashabiki milioni tano waliojisajili, na pia ana zaidi ya wafuasi wa Instagram milioni 12.

Diamond Platnumz alianzisha WCB Wasafi na kuibadilisha kuwa moja ya lebo kuu barani Afrika, ikiwa imesajili wasanii wenye mafanikio makubwa kama vile Lava Lava, Mbosso, Rayvanny na Zuchu.

Kwenye mkataba huu mpya wa kimkakati, Warner Music, Diamond Platnumz, Ziiki Media na wasanii wa WCB Wasafi watashirikiana kwenye matoleo mapya, albamu zao, pamoja na mikataba ya moja kwa moja na kampuni za biashara.

Warner Music imewahi kufanya kazi na zaidi ya wasanii 6,500, akiwemo Master KG wa Afrika Kusini anayetambulika kwa wimbo wake Jerusalema, Burna Boy na Sho Madjozi.

Diamond Platnumz ni mmoja wa wasanii waliofaulu zaidi Afrika.

CHANZO - BBC SWAHILI
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger