Bill na Melinda Gates wametangaza talaka yao baada ya miaka 27 ya ndoa, wakisema "hatuamini tena tunaweza kuwa pamoja kama wanandoa".
"Baada ya kufikiria sana na kufanya kazi nyingi juu ya uhusiano wetu, tumefanya uamuzi wa kumaliza ndoa yetu," wawili hao walisema katika ujumbe wa twitter .
Walikutana kwa mara ya kwanza miaka ya 1980 wakati Melinda alipojiunga na kampuni ya Bill ya Microsoft.
Wanandoa hao mabilionea wana watoto watatu na kwa pamoja wanaendesha Wakfu wa Bill & Melinda Gates.
Shirika hilo limetumia mabilioni kufadhili kampeni mbalimbali ikiwemo magonjwa ya kuambukizana na kuhamasisha chanjo kwa watoto.
Wawili hao - pamoja na mwekezaji Warren Buffett - wanahusika na mpango wa Ahadi ya Kutoa, ambao unawataka mabilionea kujitolea kutoa utajiri wao mwingi kwa malengo ya kuwafaidi watu .
Bill Gates ndiye mtu wa nne tajiri zaidi ulimwenguni, kulingana na Forbes, na ana mali ya thamani ya $ 124bn (£ 89bn).
Alipata pesa kupitia kampuni aliyoianzisha miaka ya 1970, Microsoft, kampuni kubwa ya programu ulimwenguni.
Wawili hao walichapisha taarifa hiyo wakitangaza talaka yao kwenye Twitter.
"Katika kipindi cha miaka 27 iliyopita, tumewalea watoto watatu wa ajabu na kujenga wakfu ambao unafanya kazi ulimwenguni kote kuwezesha watu wote kuishi maisha yenye afya, yenye tija," ujumbe huo ulisema.
"Tunaendelea kuwa na imani ya pamoja katika lengo hilo na tutaendelea kufanya kazi pamoja kwenye wakfu wetu , lakini hatuamini tena tunaweza kukua pamoja kama wanandoa katika sehemu inayofuata ya maisha yetu.
"Tunaomba nafasi na faragha kwa familia yetu tunapoanza maisha haya mapya."
Walikutanaje ?
Melinda alijiunga na Microsoft kama msimamizi wa bidhaa mnamo 1987, na hao wawili walikaa pamoja kwenye dhifa ya chakula cha jioni cha biashara mwaka huo huko New York.
Walianza kuchumbiana, lakini kama Bill alivyokiambia kipindi kimoja cha Netflix: "Tulijaliana sana na kulikuwa na uwezekano wa mawili kutokea : ama, tungeachana au tungeoana."
Melinda alisema alimpata Bill - akiwa mtu wa kawaida inaonekana hata katika maswala ya moyo - akiandika orodha kwenye ubao mweupe na "faida na hasara za kuoa".
Walioana mnamo 1994 katika kisiwa cha Lanai cha Hawaii,wakikiripotiwa kukodi helikopta zote za eneo hilo kuwazuia wageni wasiohitajika kupaa na kuja harusini mwao bila kualikwa.
Bill Gates alijiuzulu kutoka bodi ya Microsoft mwaka jana ili kuzingatia shughuli zake za uhisani.
CHANZO - BBC SWAHILI
0 comments:
Post a Comment