WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoa wa Ruvuma, Hamza Mwenda ahakikishe anawakamata madiwani na watendaji wa Halmashauri ya Mbinga Vijijini ili wajibu tuhuma za rushwa zinazowakabili.
Madiwani wa kata za Mkumbi (Bruno Kapinga), kata ya Lukalasi (Bosco Ndimbo) na wa kata ya Linda (Haule) wanadaiwa kuchukua fedha kutoka kwa watendaji wa AMCOS kwa ajili ya kwenda kushawishi kuhamishwa kwa eneo la ujenzi wa makao makuu ya halmashauri hiyo.
Ametoa agizo hilo leo (Jumatatu, Januari 4, 2021) baada ya kuzindua jengo la utawala la Halmashauri ya Mji wa Mbinga akiwa wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma. Waziri Mkuu amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Christine Mndeme asimamie ujenzi wa halmashauri hiyo unaoendelea katika eneo la Kigonsera.
Hatua hiyo imekuja baada ya kuwepo kwa mvutano wa Madiwani wa Halmashauri ya Mbinga Vijijini ambao baadhi yao hawataki makao makuu ya halmashauri hiyo yajengwe Kigonsera na kuamua kuendesha mchakato wa kushawishi wengine wagomee mradi huo jambo ambalo linakwamisha maendeleo kwa sababu tayari mradi huo umeshaanza kujengwa.
Mvutano huo unaongozwa na Madiwani wa Kata tatu za Mkumbi, Lukalasi na Linda ambao wanataka makao makuu yajengwe kwenye kata ya Mkumbi katika eneo ambalo litailazimu Serikali ilipe fidia ya zaidi ya shilingi milioni 400 huku kukiwa na eneo la bure la ekari 150 ambalo ndiko yanakojengwa makao makuu.
“Hatuwezi kukubali huko mnakotaka nyie ni lazima tulipe fidia ya zaidi ya shilingi milioni 400 na kuna eneo la bure ekari zaidi ya 150, hii haikubaliki hatuwezi kufanya mambo ya siasa kwenye fedha za wananchi haiwezekani. Mmeamua kila AMCOS ichange shilingi 600,000 mpate milioni tatu mfanye kampeni ya kutaka halmashauri ijengwe kweni hiyo ni rushwa.”
Waziri Mkuu ameongeza kuwa “Kwa kuwa zile ni fedha za wakulima, Kamanda wa TAKUKURU kawakamate watendaji wa AMCOS hizo wahojiwe kwa nini walitumia fedha za kuwapa Madiwani wakahonge ni lazima wahojiwe waeleze ni nani aliyetoa maagizo ya kutoa shilingi milioni tatu. Hatuwezi kutumia fedha za wananchi kwa ajili ya kuhonga watu lazima fedha hizo za wakulima zirudishwe ni mali ya wakulima.”
Mapema, Waziri Mkuu alizindua jengo la utawala la Halmashauri ya Mji wa Mbinga na kukagua ujenzi wa nyumba nane za watumishi wa halmashauri hiyo na amesema kwamba ameridhishwa na utekelezaji wa miradi hiyo iliyogharimu shilingi bilioni 3.7
Pia, Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kumpongeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Mbinga, Grace Quintine kwa usimamizi mzuri wa miradi hiyo ambayo imejengwa kwa viwango bora na majengo hayo yanalingana na kiwango cha fedha kilichotolewa.
“Tulimletea shilingi milioni 350 hapa kwa ajili ya ujenzi wa nyumba saba za watumishi na ametumia milioni 321 na tulimletea shilingi milioni 300 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ya Mkurugenzi lakini ametumia shilingi milioni 251 na hakuna ubabaishaji majengo yote yamejengwa kwa viwango bora. Nampongeza sana Mkurugenzi huyu amefanya vizuri sana endelea kujenga miradi mingine ikiwemo na ya vyumba vya madarasa.”
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Mbinga, Grace Quintine amesema halmashauri yao katika mwaka wa fedha 2019/2020 ilipekea shilingi milioni 650 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za watumishi zikiwemo saba za Wakuu wa Idara na moja ya Mkurugenzi.
Amesema gharama za ujenzi wa nyumba saba za Wakuu wa Idara ni shilingi milioni 321.771 ambapo kila nyumba iligharimu shilingi milioni 45.967 kati ya shilingi milioni 50 zilizoidhinishwa za kupokelewa ambapo kila nyumba ilikadiriwa kutumia shilingi milioni 350 kwa nyumba zote.
“Ujenzi wa nyumba ya ghorofa moja ya Mkurugenzi wa Mji umegharimu shilingi milioni 251.780 kuhu makadirio yakiwa ni shilingi milioni 300. Lengo la miradi hii ni kuboresha mazingira ya makazi ya watumishi wa halmashauri ikiwa ni pamoja na kupunguza kilipa posho za nyumba kwa kila mwezi.”
Amesema shilingi milioni 28.228 zilizobaki katika ujenzi wa nyumba za Wakuu wa Idara zitatumika kujenga mnara wa tenki la maji na uwekaji wa tenki moja la maji kwa kila nyumba na kuanza ujenzi wa uzio kuzunguka nyumba zote saba.
Mkurugenzi huyo amesema mbali na utekelezaji wa ujenzi wa miradi hiyo ya nyumba za makazi, pia Serikali ilitoa shilingi bilioni 3.1 kwa ajili ya ujenzi wa jengo la utawala la halmashauri hiyo ambalo lilijengwa na kampuni ya SUMA-JKT Kanda ya Mtwara.
Amesema ujenzi wa jengo hilo la utawala lenye jumla ya vyumba 52 vikiwemo vyumba vya ofisi za watumishi na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji, ukumbi mkubwa wa mikutano na ukumbi mdogo kwa ajili ya vikao vya Wakuu wa Idara na Vitengo. “Ujenzi umekalika na lilianza kutumika Januari 2020. Naishukuru Serikali kwa utekelezaji wa miradi hii.”
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
0 comments:
Post a Comment