Saturday, 30 January 2021

Naibu Waziri Ummy- Watu Wenye Ulemavu Changamkieni Asilimia 2 Ya Mikopo Inayotolewa Na Serikali

...


Na: Mwandishi Wetu
Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Watu wenye Ulemavu Mhe. Ummy Nderiananga amewataka Watu wenye Ulemavu kuchangamkia fursa ya mikopo ya asilimia 2 inayotolewa na Halmashauri zilizopo nchini kupitia asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri (4% Wanawake, 4% Vijana na Watu wenye Ulemavu 2%) ili waweze kuanzisha miradi mbalimbali itakayowainua kiuchumi.

Ameeleza hayo wakati wa ziara ya kikazi Mkoani Mara alipokutana na kufanya mazungumzo na Viongozi wa Mkoa huo pamoja na Viongozi wa vyama vya Watu Wenye Ulemavu katika Mkoa huo, Mheshimiwa Ummy alieleza kuwa watu wenye ulemavu wanatakiwa kuchangamkia fursa ya mikopo ambayo wanatengewa na serikali kwa kuwa mikopo hiyo haina riba ili ziwasaidie kuboresha Maisha yao kupitia miradi mbalimbali watakayoianzisha.

“Mkiwa kama viongozi wa Vyama vya Watu wenye Ulemavu hakikisheni mnahamasisha wenzenu kuanzisha vikundi ili muweze kuchangamkia fursa ya mikopo hii inayotolewa na serikali ili muweze kuanzisha shughuli zitakazo waletea maendeleo,” alieleza Ummy

“Nimefurahishwa kuona Mkoa wa Mara umekuwa mstari wa mbele katika kuwawezesha watu wenye ulemavu kupata mikopo hiyo, zaidi ya milioni 115,226,660 zimeweza kutolewa kwenye vikundi mbalimbali vya watu wenye ulemavu vilivyopo kwenye mkoa huu, ninawapongeza sana uongozi wa mkoa kwa jitihada hizo,” alisema Naibu Waziri Ummy

Alieleza kuwa, Serikali ina dhamira ya dhati na nia njema kwa Watu wenye Ulemavu hivyo ilitoa fursa ya mikopo hiyo ya asilimia 2 ili wenye ulemavu na wao waweze kupata fursa ya kufanya shughuli mbalimbali zitakazo wawezesha na wao kuchangia katika pato la taifa.

“Mnafahamu kuwa serikali yetu imeingia kwenye uchumi wa kati na dhamira ya serikali ni kukuza uchumi wake kupitia viwanda, hivyo ni vyema watu wenye ulemavu wakatumia fursa hiyo ya mikopo ya asilimia 2 inayotolewa na halmashauri ili na nyie muanzishe viwanda vidogo vidogo, uwezo huo mnao,”

“Mmemsikia Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli anataka nchi hii iwe na mabilionea wengi, kati ya hao mabilionea natamani kuona na watu wenye ulemavu mkiwemo uwezo huo natambua mnao kwa kuwa mnaweza kufanya mambo makubwa na yakawashangaza watu wengi kwamba watu wenye ulemavu wanaweza kama wengine wasio na ulemavu,” alisema Mheshimiwa Ummy

“Maafisa Ustawi wa Jamii hakikisheni mnawasaidia watu wenye ulemavu wanapokuja katika ofisi zenu na mawazo au maandiko ya kuanzisha biashara au miradi mbalimbali ya uzalishajimali ili waweze kupata mikopo ya asilimia 2 waliyotengewa,” alisema

Alifafanua kuwa, Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli imekuwa ikiwajali watu wenye ulemavu sambamba kuboresha huduma za msingi za kundi hilo, huku akielezea pia juu ya namna uzingatiwaji huo kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi katika Ibara ya 94, 95 na 96 ambazo zinaelezea na kufafanua mwelekeo wa namna masuala ya Watu wenye Ulemavu yatakavyokuwa yakishughulikiwa, kuendelea kutambua na kuwapatia kipaumbele katika masuala mbalimbali ya kimaendeleo.

Sambamba na hayo, Naibu Waziri Ummy alihimiza juu ya Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya kujumuisha masuala ya wenye ulemavu kwenye Mabaraza ya mashauriano ya Mkoa (Regional Consultative Councils) na Mabaraza ya Mashauriano ya Wilaya (District Consultative Councils) ili waweze kutambua mahitaji yao ikiwemo kuwapatia huduma bora, haki zao za msingi kwa lengo la kuimarisha ustawi wao, kuimarishwa kwa huduma za afya na zenye staha kwa watu wenye ulemavu wa kila aina, kuimarisha ulinzi, kuendelea kuwawezesha watu wenye ulemavu kiuchumi, kuwapatia elimu kwa kuimarisha elimu jumuishi, kujengwa kwa miundombinu fikivu na kuendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusiana na masuala mbalimbali ya wenye ulemavu.

Aidha, Mheshimiwa Ummy amewataka pia Viongozi wa Vyama vya Watu wenye Ulemavu kuimarisha ushirikiano baina yao na viongozi wa mkoa kwa kuwa na upendo na amani ili waweze kujadiliana na kushauriana masuala mbalimbali yanayohusu Watu wenye Ulemavu.

Sambamba na hayo, Naibu Waziri Ummy alitoa wito kwa jamii kuacha kuwanyanyapaa na kuwaficha watu wenye ulemavu badala yake wawaibue na kuwaunganisha na fursa mbalimbali katika jamii.

Naye, Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Mhe. Karolina Mthapula alisema kuwa Mkoa wa Mara utaendelea kutoa hamasa kwa watu wenye ulemavu kujitokeza na kuchangamkia fursa mbalimbali zinazotolewa kwa ajili ya watu wenye ulemavu.  

Pia, alieleza uongozi wa Mkoa utaendelea kushirikiana na Viongozi wa Vyama vya Watu wenye Ulemavu katika mkoa huo pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama, mamlaka za serikali za mitaa kuhakikisha watu wasio waadilifu katika jamii na wenye nia ovu katika kuwatumia watu wenye ulemavu wanachukuliwa hatua za kisheria.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Shirikisho la Watu wenye Ulemavu Mkoa wa Mara, Ndg. Iddy Mtani alitumia fursa hiyo kuishukuru Serikali namna inavyowajali Watu wenye Ulemavu na alieleza kuwa vikao ambavyo amekuwa akifanya Naibu Waziri anayeshughulikia masuala ya watu wenye ulemavu vitaleta tija na kuongeza uelewa wa masuala ya watu wenye ulemavu hususan kwa jamii na viongozi katika kutambua namna watakavvyokuwa wakishirikiana kwa pamoja katika kuendesha gurudumu la maendeleo.

Katika Ziara hiyo Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Watu wenye Ulemavu Mhe. Ummy Nderiananga alitembelea Shule ya Mingi Msingi ya Mwisenge iliyopo mkoani Mara kwa lengo kujionea mazingira na miundombinu fikivu iliyojengwa katika shule hiyo kwa ajili ya kuwawezesha watu wenye ulemavu kupata elimu bora. Aidha Shule hiyo ya Msingi ya Mwisenge ina historia kubwa katika kataifa ambapo Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerer alisoma katika shule hiyo.


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger