Na. Edward Kondela
Jeshi la polisi Mkoa wa Arusha kwa kushirikiana na Wizara ya Mifugo na Uvuvi pamoja na vyombo vingine vya ulinzi na usalama tarehe 27.01.2021 limewakamata watuhumiwa watatu kwa tuhuma za wizi na utoroshaji wa mifugo maeneo ya mipakani.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa mwishoni mwa wiki na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Kamishna Msaidizi wa Jeshi la Polisi Salum Hamduni amesema jeshi hilo limewakamata watuhumiwa hao katika tarafa ya Loliondo, Wilaya ya Ngorongoro mkoani humo kufuatia agizo alilolitoa Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki Jumatano iliyopita la kukamatwa kwa watuhumiwa 67 wa utoroshaji wa mifugo na mazao yake.
Kamanda Hamduni amesema kukamatwa kwa watuhumiwa hao watatu kunatokana na baada ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kutangaza operesheni ya kudhibiti wizi na utororshaji wa mifugo maeneo ya mipakani ambapo zilipatikana taarifa za uwepo wa watu wanaojihusisha na wizi na utoroshaji wa mifugo katika Wilaya ya Ngorongoro.
Ameongeza kuwa upelelezi bado unaendelea kuhusiana na tukio hilo, mara utakapokamilika jalada litapelekwa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kwa ajili ya hatua zaidi za kisheria.
Ametoa wito kwa wananchi kuepuka usumbufu kwa kuhakikisha wanafuata sheria za biashara ya usafirishaji wa mifugo kwani wasipofanya hivyo watakamatwa na kuchukuliwa hatua kali za kisheria.
Jumatano ya wiki iliyopita Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki akiwa katika ofisi za wizara hiyo zilizopo katika mji wa serikali Mtumba jijini Dodoma wakati akiwasilishiwa ripoti ya uchunguzi, kuhusu utoroshaji wa mifugo mipakani aliliagiza Jeshi la Polisi nchini Kikosi cha Kuzuia Wizi wa Mifugo kuwakamata mara moja watuhumiwa 67 wa utoroshaji wa mifugo na mazao yake kwenda nchi za jirani.
Katika ripoti ya uchunguzi, kuhusu utoroshaji wa mifugo mipakani, iliyowasilishwa na Kamishna Msaidizi wa Jeshi la Polisi Julius Mjengi kwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki imeeleza kuwa kabla ya tarehe 7 Novemba, 2020, mifugo iliyokuwa inatoka kwenye minada ya awali ya Handeni na Kilindi kuelekea nchini Kenya kupitia mpaka wa Horohoro haikuwa inafuata taratibu za forodha kama shehena nyingine.
Aliongeza kuwa takwimu za daftari la mifugo katika mpaka wa Horohoro zinaonyesha idadi ya mifugo iliyopitishwa kuelekea nchini Kenya kwa kipindi cha miaka 17 kutoka mwaka 2003 hadi Novemba, 2020 ilikuwa ni ng’ombe 24,980 na Mbuzi na Kondoo 9,368 (sawa na wastani wa Ng’ombe 122 na Mbuzi/Kondoo 46 kwa mwezi).
Taarifa hiyo ilibainisha pia baada ya uchunguzi, ilionekana kuwa kati ya tarehe 7 Novemba, 2020 hadi tarehe 9 Desemba, 2020 (kipindi cha mwezi mmoja tu) jumla ya Ng’ombe 1,096 na Mbuzi na Kondoo 1,044 walipitishwa katika kituo cha Forodha kuelekea nchini Kenya, ambapo huo ni wastani wa idadi ya mifugo iliyopita mpakani ndani ya mwezi mmoja ukilinganisha na siku za nyuma.
Taarifa imebaini pia viashiria vya udanganyifu wa kurekodi idadi sahihi ya mifugo inayokaguliwa kwenda Kenya hususan katika mpaka wa Hororohoro – Tanga.
Mwisho.
Imetolewa: Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Mifugo na Uvuvi
30.01.2021
0 comments:
Post a Comment