Wizara ya Kilimo imesema katika bajeti ya mwaka 2021/22 inatarajia kutenga fedha mahsusi kwa ajili kugharimia huduma za ugani ili kuondoa changamoto zinazotatiza ukuaji wa tija kwenye uzalishaji mazao nchini ikiwemo maslahi ya maafisa kilimo ugani.
Waziri wa Kilimo Prof. Adolf Mkenda ametoa kauli hiyo jana (30.01.2021) jijini Dodoma wakati akifunga kikao kazi baina ya wizara yake na maafisa kilimo toka mikoa 26 na halmashauri zote 185 za Tanzania bara uliojadili hali ya upatikanaji huduma za ugani kwenye kilimo.
“Kilimo kimekuwa na maneno mengi utasikia kilimo ni uti wa mgongo ama kilimo cha kufa na kupona.Sasa tunasema maneno yametosha hebu tuanze hatua moja mbele kwa vitendo tuboreshe utoaji huduma za ugani nchini ili wakulima wahudumiwe kwa vitendo” alisema Prof. Mkenda.
Prof. Mkenda alibainisha kuwa wizara yake imeitisha kikao hicho cha siku mbili ili kujadiliana na wataalam wa kilimo wote pamoja na wadau wa sekta binafsi hali ya kuboresha utoaji huduma za ugani na kuweka mikakati ya kuondoa changamoto za ugani
Alisema kuwa suala la kutokuwepo bajeti mahsusi kwa ajili ya watoa huduma za ugani kwenye ngazi za mikoa, halmashauri na vijiji imekuwa ikiathiri utoaji huduma kwa wakulima kushindwa kulima kwa tija.
Katika kikao hicho Waziri wa Kilimo alirejea kueleza dira ya wizara yake kwa sasa na kutaja mambo manne ya kipaumbele ili kilimo kichangie zaidi ukuaji wa uchumi kwanza ni kuongeza utafiti na uzalishaji mbegu bora za mazao.
Pili, kutoa elimu bora ya kilimo ,tatu kutafuta masoko ya mazao ya wakulima na nne kuhakikisha wakulima na wawekezaji wanapata mitaji yenye riba nafuu toka kwenye taasisi za kifedha nchini.
“Tutawekeza fedha bajeti ijayo na nguvu kukuza utafiti ili tupate mbegu bora zaidi zenye kutoa mavuno bora na tija kwa wakulima” alisisitiza Prof. Mkenda.
Kwa upande wake Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji Charles Mwijage alisema anawapongeza wakulima wa Tanzania pamoja na wataalam wa kilimo kwa kuhakikisha katika kipindi cha miaka mitano ya kwanza ya serikali ya awamu ya tano Tanzania haikupata tatizo la njaa.
“ Kipindi chote kuanzia mwaka 2015 hadi 2020 nchi hii haikupata njaa, tunawashukuru maafisa ugani na wakulima wote wa Tanzania kwa kazi kubwa ya kuhakikisha taifa lina chakula cha kutosha” alisema Mwijage ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Viwanda na Biashara.
Mwijage aliiomba serikali kuweka mikakati mizuri na kuongeza bajeti ya kuhudumua watoa huduma za ugani wa serikali waliopo chini ya Ofisi ya Rais Tamisemi na Wizara ya Kilimo ili watatue changamoto za wakulima.
Naye Mwenyekiti wa umoja wa Maafisa Kilimo Halmashauri (DAICOs) Enock Ndunguru aliomba serikali kupitia Wizara ya Kilimo kuwa na mkakati wa kuwahamishia maafisa ugani waliopo halmashauri zote nchini kutoka Mamlaka za Serikali za Mitaa na sasa wawe chini ya Wizara ya Kilimo.
Katika hatua nyingine Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya alisema kwa sasa kuna maafisa ugani kilimo 6700 ambao wanahitaji kuwezeshwa vitendea kazi ili watekeleze majukumu yao ya kusimamia kilimo
Kusaya alisema kwa kuanzia wizara ya kilimo itaendeleza mkakati wa kuwapatia pikipiki maafisa ugani wote 67000 kwa awamu pamoja na kupeleka kifaa maalum cha kupima afya ya udongo (Extension Kit).
Akizungumza kwenye kikao hicho Mbunge wa Musoma Vijijini Prof. Sospeter Muhongo alitoa wito kwa serikali kufanya jitihada za kukifanya Chuo Kikuu cha Kilimo cha Mwalimu Nyerere (Mwalimu Nyerere University of Agriculture) kilichopo Butiama Mara kianze kudahili wanafunzi mwaka 2021/22 ili kifundishwe maafisa ugani.
“Chuo hiki cha Kilimo cha Mwalimu Nyerere cha Butiama kimekusudiwa kufundisha wataalam wa ugani ,tunaomba kianze mapema mwaka huu 2021 ili tatizo la upatikanaji wataalam wa kilimo hususan vijijini litatuliwe” alisema Prof. Muhongo.
Mwisho
Imeandaliwa na;
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Kilimo
DODOMA
31.01.2021
0 comments:
Post a Comment