Wadau wa Habari wa Kanda ya Ziwa wameahidi kuendelea kufanya kazi kwa ukaribu na vyombo vya Habari Nchini ili kuifikia jamii na kuihabarisha juu ya shughuli wanazofanya.
Hayo yamesemwa kwenye mkutano wa vyombo vya habari uliondaliwa na Klabu ya Waandishi wa Habari ya Mkoa wa Mwanza (MPC) kuelekea tukio la hafla ya usiku ya Waandishi wa habari na wadau wa Habari iliyopangwa kufanyika Februari 1 mwaka huu.
Mwakilishi wa NHIF Paul Bulolo alisema kuwa, Vyombo vya Habari na Waandishi wa habari wamekuwa na mchango mkubwa kwa kuwa daraja la kufikisha taarifa kwa jamii zinazofanywa na NHIF juu huduma za afya.
Naye Mkurugenzi wa shirika la EMEDO Editrudith Lukanga amesema kuwa, Waandishi wa Habari wana nafasi kubwa ya kufikisha taarifa kwa jamii na hivyo kuwaomba waandishi kupitia klabu ya Mwanza kushirikiana na EMEDO ili kujua programu zinazowagusa wanawake na vijana zinavyotekelezwa.
Kuwa upande wake, Mkurugenzi wa Yuhoma Education Limited Bwana Yussuf Yuhoma amesema kuwa, vyombo vya habari vinafanya kazi kubwa hasa kwenye kuemimisha, kuhabarisha na kuburudisha hivyo amesema wataendelea kufanya kazi na waandishi wa habari.
Bwana Makwaya Makani kutoka kampuni ya Jambo alisema kuwa, kampuni yao inatambua mchango wa vyombo vya habari na hata wao wana mpango wa kufungua kituo cha redio kitakachoitwa Jambo FM ili kuchangia maendeleo ya Taifa na kufanya kazi na klabu ya Waandishi ya Mwanza kwa ukaribu.
Mwakilishi wa kampuni ya bia ya TBL Diamond Mawai alisema kuwa,wao walianza zamani kufanya kazi na waandishi wa habari hivyo anatambua umuhimu wao na wataendelea kutoa ushirikiano wa kutosha.
Bwana Kalebe Luteli mwakilishi toka Hospitali ya Bugando ameweka wazi kwamba kwenye sekta ya afya Bugando imefanya mambo makubwa kupitia ushirikishwaji wa waandishi wa habari hivyo wataendelea kufanya kazi kwa karibu na waandishi.
Naye Mwenyekiti wa MPC bwana Edwin Soko alisema kuwa, wadau wa habari wasiviogope vyombo vya habari kwani waandishi wa habari sio maadui wa wadau wa habari bali ni marafiki zao.
Soko aliongeza kuwa, kukiwepo ushirikiano baina ya wadau wa habari na vyombo vya habari basi ni rahisi wananchi kupata maendeleo.
Usiku wa waandishi wa habari na wadau wa habari utafanyika Februari 1 kwenye Hotel ya Gold Crest Mwanza.
0 comments:
Post a Comment