Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na wananchi wa Chapulwa Kahama mara baada ya kuweka jiwe la msingi ujenzi wa Kiwanda cha Nafaka, Vinywaji na Maziwa (Kom Limited) Kahama mkoani Shinyanga leo tarehe 28 Januari 2021. Picha na Ikulu
***
Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli ameipandisha hadhi halmashauri ya Kahama Mji kuwa Manispaa ambapo sasa Kahama Mji itajulikana kama Manispaa ya Kahama.
Rais Magufuli amesema hayo leo Alhamis Januari 28,2021 wakati akizungumza na wananchi katika uwanja wa taifa wilayani Kahama.
"Kutokana na mahitaji yaliyopo hapa Kahama naipandisha halmashauri ya Kahama Mji kuwa Manispaa na hiyo hospitali ya Kahama iwe na hadhi ya Manispaa",amesema Rais Magufuli.
Mkoa wa Shinyanga sasa utakuwa na Manispaa mbili (Manispaa ya Shinyanga na Manispaa ya Kahama), lakini pia kuwa na halmashauri za wilaya nne ambazo ni halmashauri ya wilaya ya Kishapu, Shinyanga, Ushetu na Msalala.
Rais Magufuli pia amemsamehe Mkurugenzi wa Kahama Mji, Underson Msumba ambaye ni miongoni mwa wakurugenzi wanne waliokuwa na kashfa kwa kununua magari ya kifahari ambapo amesema amemsamehe na kumuachia gari hilo kutokana na jinsi anavyofanya kazi vizuri na kwa kujituma akishirikiana na madiwani ambapo wamekuwa wakitekeleza miradi yenye kuwaletea maendeleo wananchi.
"Mkurugenzi wa Kahama Mji unafanya kazi kubwa sana, ka kosa kale kadogo kamesamehe dhambi zako zote. Unafanya kazi sana japo unapigwa vita sana. Nimemsamehe Mkurugenzi huyu, amefanya makubwa! Mkurugenzi hongera Sana. Na hilo gari nitamrudishia aendelee kuliendesha lakini asirudie kununua gari nje ya utaratibu",amesema Magufuli.
Rais Magufuli pia amemuagiza Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Doroth Gwajima kuipandisha hadhi hospitali ya Mji Kahama iendane na hadhi ya Manispaa.
"Nawaongezea Sh Milioni 500 kuchangia jengo la hospitali ya mji Kahama. Na kwa vile waziri wa afya yuko hapa aipandishe hadhi hiyo hospitali ili endane na hatua ya Manispaa," amesema Rais Magufuli.
0 comments:
Post a Comment