Wednesday, 27 January 2021

WAITARA AMTAKA DED TARIME KULIPA DENI LA MIL.185 LINALODAIWA NA MSD NA KUSABABISHA KUTOPATIWA DAWA

...

Mbunge wa jimbo la Tarime vijijini ambaye pia ni Naibu Waziri Ofisi ya Rais,Muungano na Mazingira Mwita Waitara akizungumza na wagonjwa waliofika katika kituo cha afya Nyangoto wakati wa ziara yake ya kutembelea kituo kubaini changamoto. Picha na Dinna Maningo.
Mbunge wa jimbo la Tarime vijijini ambaye pia ni Naibu Waziri Ofisi ya Rais,Muungano na Mazingira Mwita Waitara akizungumza na wagonjwa waliofika katika kituo cha afya Nyangoto wakati wa ziara yake ya kutembelea kituo kubaini changamoto. Picha na Dinna Maningo.
Veronica Tontora mwenyekiti wa kitongoji cha Lamboni akionyesha eneo ambao limetelekezwa kwa zaidi ya mwaka mmoja ambalo lilikuwa linatumika wagonjwa na wanaojifungua kufua nguo zao lakini halitumiki kwa madai limeziba.
Katibu wa Chama cha Mapinduzi(CCM) wilaya ya Tarime mkoani Mara Hamis Mkaruka akitizama eneo hilo.

Na Dinna Maningo,Tarime.
Hali ya upatikanaji wa dawa kwenye zahanati na vituo vya afya katika halmashauri ya wilaya ya Tarime imekuwa gumzo kila kona jambo ambalo limekuwa kero kwa wananchi wanapokwenda kupata huduma ya afya baadhi ushindwa kumudu gharama za dawa kwenye maduka binafsi ya dawa kutokana na kuwa na gharama kubwa.

Kufuatia uhaba huo wa dawa mbunge wa jimbo la Tarime vijijini ambaye pia ni Naibu Waziri Ofisi ya Rais,Muungano na Mazingira Mwita Waitara amemtaka mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Tarime Apoo Tindwa kuhakikisha halmashauri inalipa deni la shilingi mil.185 inayodaiwa na Bohari ya dawa (MSD) ili kunusuru afya za wananchi wanaopata huduma za afya katika zahanati na vituo vya Serikali.

Waitara aliyasema hayo wakati alipokitembelea kituo cha afya Nyangoto- ili kujionea huduma zinazotolewa baada ya kupata taarifa kutoka kwa wananchi wake kuhusu kituo hicho kukabiliwa na changamoto zikiwemo za ukosefu wadawa,gharama za kitandani, gharama za mgonjwa afikishwapo kituoni hapo, wanaojifungua kwenda na nguo kufua nyumbani,gharama za vipimo,ukosefu wa gari la wagonjwa.

Wakieleza kero zilizopo, Diwani wa viti maalumu Ferister Julius alisema kuwa kituo hicho hakina dawa na baadhi ya vifaa tiba na kila anaopofatilia kujua sababu ya kutokuwepo kwa dawa uelezwa kuwa hakuna dawa kwakuwa kituo hicho kina deni la dawa.

"Hali ya huduma kwenye kituo ni mbaya kila kitu ni chakununua ,nilileta mgonjwa hata karatasi za kuandikia hakuna nikaambiwa nikanunue daftari,ukileta mgonjwa unalipia sh.5,000/= , kitanda 5,000/= kila kipimo unalipia sh.2,000/= bado unaambiwa ununue dawa,bado mabomba ya sindano,gloves hii ni kero wagonjwa wanapata tabu nilipofuatilia kwa DMO nikaambiwa kuwa kituo kina deni la dawa ndiyo maana hakuna dawa japo sikufahamu ni deni la shilingi ngapi",alisema.

Diwani wa viti maalumu Elizabeth Marembera alisema kuwa ukosefu wa dawa umesababisha wananchi kugoma kujiunga na mfuko wa afya ya jamii ICHF na na mfuko wa bila ya afya NHIF kwakuwa hata walio na bima ujigharamikia dawa kwa fedha zao hali ambayo imesababisha wananchi kutoshawishika kujiunga.

Diwani wa kata ya Kemambo Rashid Bogomba aliongeza, "Kuna hospitali zingine ukienda huna bima wanakushangaa lakini ukiwa na bima wanakujali kama mfalme shida ya hapa wao wanajali watu wanaotoa fedha kuliko watu wenye bima".

Diwani wa kata ya Matongo Godfrey Kegoye alisema kuwa huduma ya afya ni hafifu ambapo wodi ya wanawake ina upungufu wa vitanda na kusababisha wagonjwa wawili kuchangia kitanda kimoja na wakiwa wengi wengine ulala chini hali inayosababisha watu kukikimbia kituo hicho cha serikali nakwenda kupata huduma kwenye zahanati na vituo binafsi.

Licha ya kuwepo kwa gari lililoandikwa kituo cha afya Nyangoto lakini limekuwa halikai muda wote kituoni, mgonjwa akipewa rufaa ndugu hulazimika kutumia usafiri wa gari za kukodi na wasio na fedha hupoteza maisha.

Wambura Machugu Mwenyekiti wa kitongoji cha Kebamonche na mjumbe wa kamati ya afya na mazingira kijiji cha Mjini Kati alisema kuwa kukosekana kwa gari la wagonjwa baadhi ya wagonjwa wanaopata rufaa kwenda hospitali ya wilaya,mkoa na Bugando hufariki kwa kuwa wengine wanashindwa kumudu gharama za usafiri.

“Juzi kuna mgonjwa alilazwa hapa kituoni alikaa siku mbili hali yake ilikuwa mbaya ikatakiwa asafirishwe kwenda mkoani lakini hapakuwa na gari hali ikawa mbaya akafia hapa kituoni,na hapa sasa hivi hakuna damu ukiishiwa damu unaambiwa uende hospitali ya wilaya au mkoani, hii inaumiza kituo kikubwa kama hiki kina gari lakini gari linakwenda kufanya kazi kwingine nawakati lililetwa kwa matumizi ya kituo hiki", alisema.

Mjumbe wa serikali ya kijiji cha Mjini Kati ambaye pia ni Mwenyekiti wa umoja wa wanawake Tanzania (UWT) kata ya Matongo Pendo Mnata alisema kuwa baadhi ya watoa huduma wakiwemo wauguzi wamekuwa na kauli mbaya kwa wagonjwa wakiwafoka na wakati mwingine kupuuza shida zao,aliwataka kuzingatia maadili ya kazi zao na kuwa na lugha rafiki kwa wagonjwa.

Mwenyekiti wa kitongoji cha Lamboni Veronica Tontora alisema"akina mama wakijifungua unaambiwa uondoke na nguo ukafulie nyumbani kuna mmoja alinieleza kuwa alipojifungua aliambiwa aondoke na kondo na nguo akafulie kwake,hakuna sehemu ya kufua nguo unapokuwa umejifungua hata wagonjwa wengine wanateseka tunaomba huduma ziboreshwe".

Mwenyekiti wa kamati ya Afya kituo cha afya Nyangoto,Isaack Zabroni alisema eneo lililotengwa kwa ajili ya kufua nguo za wanojifungua na wagonjwa lina mwaka mmoja halitumiki hivyo watu ulazimika kufua katika bafu zilizopo kituo cha afya pindi wanapooga na kwamba hakuna akina mama wanaokwenda kufua nguo nyumbani kwa kuwa hufua kwenye bafu wakati wanapooga.

"Ni mwaka mmoja sinki halitumiki lilitengenezwa chini ya kiwango na kampuni ya Kemambo iliyokuwa na zabuni ya kufanya usafi kwenye kituo cha afya wakaweka tundu dogo likaziba ili lizibuiwe mpaka lichimbwe shimo ambao watu wakifua maji yanatiririka kwenda ndani ya shimo tofauti na hapo hata likizibuliwa litachukua muda mfupi na kuziba",alisema.

Akizungumzia ukosefu wa dawa aliongeza "MSD iliingia mkataba na serikali sasa inadaiwa fedha za dawa haijalipa na hata dawa zikija zile zenye umuhimu haziletwi hii inasababisha baadhi ya wauguzi kuja na dawa zao kwaaji ya kuwauzia wagonjwa kama kuwarahisishia wagonjwa wakiona nesi kamwambia kuwa hakuna dawa alafu anamwambia atoe pesa na kumuuzia anaona kama anauziwa dawa za serikali".

“Kuna baadhi ya wauguzi walikuwa wanakuja kituoni wakiwa na mabegi yenye dawa hii ilitupa wasiwasi kujua je kweli ni dawa zao binafsi au wanachukua za kituoni ilitubidi tuzuie hilo zoezi tukakataa hakuna nesi kumwelekeza mgonjwa duka la kununua dawa au muuguzi yeyote kuuza dawa na wengine walihamishwa”,alisema Zabroni.

Mganga Mfawidhi wa kituo cha afya Nyangoto Dk. Josephat Kirambo alisema kuwa kituo hicho kimeanzishwa mwaka 1987,kwa mujibu wa sensa ya 2012 kituo kina hudumia wakazi 30,110 kutoka kata mbili ya Matongo na Kemambo zenye jumla ya vijiji nane.

Kirambo alisema kuwa mbali na huduma kwa vijiji hivyo inahudumia vijiji jirani vinne ambavyo ni Nyakunguru,Nyarwana,Nkerege,Weigita kata ya Kibasuka,kwa kata ya Nyarukoba ni Msege,Genkuru,Komarera,Nyabirongo na wilaya ya jirani ya Serengeti katika kijiji cha Nyiboko,Borega,Nyamitita,na Nyansurura kutoka wilayani Serengeti.

Mganga huyo alisema kuwa kituo hicho kina watoa huduma ya afya 38 ,kina changamoto ya upungufu wa dawa kituoni,upungufu wa watumishi, ukosefu wa duka la dawa la kituo na ICHF kuwa chini kwa kuwa na kaya 31 kwa kipindi cha miezi 6.

Akizungumzia juu ya wanaojifungua kuondoka na nguo kwenda kufua nyumbani alisema "Ile sehemu ya kufulia nguo maji machafu yaliziba watu walikuwa wanaweka nepi na vitambaa wanashindilia mle ndani ya tundu la kwenye sinki,tulielekeza namna ya kufanya usafi wakati tunaandaa sehemu nyingine na wakati mwingine nilikuwa nasimamia mimi mwenyewe lakini hawakuelewa.

“Tulielekeza kama unafua nguo za uzazi zenye damu nyingi kusanya zile damu pamoja ziwekwe kwenye shimo la pracenta lakini haikuwezekana,siamini kama mtu aliambiwa akafulie nyumbani kama yupo aliyewaambia kwakweli alifanya makosa tunaomba mtusamehe halitajirudia tena na sina taarifa ya mtu kuambiwa aondoke na kondo hakuna aliyenilalamikia”,alisema Mganga mfawidhi.

Akizungumzia suala la wagonjwa kutozwa sh.5,000/= ya kitanda,2,000/= za vipimo, 5,000/= kwa wagonjwa alisema :"Ni kweli wanachangia 5,000/= ya usajili wa mgonjwa,vipimo elfu 2,000 kila kipimo na 5,000/= ya kitanda huu ni utaratibu mpya tulioelekezwa baada ya kuwepo kwa upungufu wa dawa tulipewa maagizo na halmashauri na sisi ni kusimamia na malipo yote yanapitia kwenye mfumo”.

Alisema kuwa kituo hicho hakipati dawa kwa kuwa kilikuwa kinadaiwa deni milioni 82 na kituo kupitia mapato ya ndani kimelipa deni sh.mil.27 na kubaki na deni la mil.55 hali ambayo imesababisha kutokuwa na mahusiano mazuri na wagonjwa pale wanapokosa huduma ya dawa.

Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Tarime Apoo Tindwa alisema kuwa upungufu wa dawa ni kwenye zahanati na vituo vyote vya afya ambapo halmashauri inadaiwa deni la dawa na MSD sh.mil.185 na wanajitahidi kuhakikisha deni linalipwa.

“Zahanati ya Kerende itapandishwa hadhi na kuwa kituo cha afya,zahanati ya Itandora inaelekea kukamilika na Genkuru ili kupunguza wimbi la wagonjwa kituo cha afya Nyangoto,tunachangamoto ya gari la wagonjwa kwenye vituo tuna gari moja la kituo cha Nyangoto linalolazimika kutoa huduma na kwenye vituo vingine”,alisema Tindwa.

Mbunge Waitara alimtaka mkurugenzi kuhakikisha yanafanyika mabadiliko makubwa ya usimamizi wa huduma ya afya kikiwemo kituo cha Nyangoto ili kuondoa malalamiko mengi ya wananchi ambao wengi wao wanaopata huduma kwenye vituo vya serikali ni watu wenye uwezo wa chini wa kipato.

Waitara alisema kuwa wananchi wasipopata huduma vizuri uisema vibaya serikali na chama jambo ambalo halimpendezi nakwamba kazi yake ni kuhakikisha anatatua kero za wananchi ili zinatafutiwa ufumbuzi.

Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger