*******************************************
Taasisi ya Mifupa Muhimbili- MOI Imeandika Historia ambapo kwa mara ya kwanza imeanza kutoa huduma ya uchunguzi wa mishipa ya damu kwenye ubongo bila kufungua fuvu la kichwa katika maabara ya kisasa ya upasuaji wa ubongo (Angio Suite).
Uchunguzi huo umefanywa kwa masaa 3 na jopo la madaktari bingwa, wauguzi, watalamu wa radiolojia wazalendo 6 kutoka MOI, MNH,JKCI pamoja na hospitali ya Aghakhan. Mkurugenzi Mtendaji wa MOI Dkt Respicious Boniface amesema kuanza kwa maabara hii ni ishara ya mageuzi makubwa katika sekta ya afya hapa nchini kwani maabara ya kisasa kama hii haipo kwenye nchi nyingine kwenye ukanda wa afrika mashariki kati.
“Leo ni siku ya furaha sana kwani tumeanza kutumia maabara yetu ya upasuaji wa ubongo (Angio suite) ,hii imewezekana kutokana na dhamira ya dhati ya Mh Rais Dkt John Pombe Magufuli ya kuboresha huduma za afya hapa nchini kwani maabara hii imejengwa Serikali ya awamu ya Tano kwa zaidi ya Tsh Bilioni 7.9, kwakweli tunamshukuru sana Mh Rais” Alisema Dkt Boniface
Kwa upande wake Daktari bingwa wa upasuaji wa Ubongo MOI Dkt Lemery Mchome amesema kuanza kwa maabara hii kumeleta mageuzi makubwa katika huduma za uchunguzi na upasuaji wa ubongo hapa nchini kwani hakuna mgonjwa atakayelazimika kwenda nje ya nchi kufuata huduma hii ambayo ilikuwa haipatikani hapa nchini.
“ Tunashukuru upasuaji umefanyika salama na kwa mafanikio makubwa, tumeweza kufika kwenye ubongo wa mgonjwa bila kufungua fuvu, tumefanya upasuaji huu katika mazingizra mazuri kwani mitambo hii ni ya kisasa sana, kama mnavyoona mgonjwa yuko macho na anaongea vizuri kabisa ,hana kovu wala maumivu, hii ni hatua kubwa sana kwetu kama wataalamu.
Mgonjwa aliyefanyiwa upasuaji huo Bwana Hafidhi saidi kutoka mkoani Singida amemshukuru Mungu kwa huduma aliyopata kwani amakuwa akipata maumivu kwa kipindi kirefu bila kujua anasumbuliwa na ugonjwa gani.
“Namshukuru sana Mh Rais Dkt John Pombe Magufuli kwa kununua vifaa hivi ambavyo vimesaidia leo nimehudumiwa hapa MOI, Nawashukuru madaktari na wataalamu wote walionihudumia, nimefurahi sana na nawaambia watanzania wenzangu wenye shida kama yangu waje wahudumiwe hapa MOI,” Alisema Hafidhi
Huyu ni mgonja wa kwanza kupata huduma katika maabara hii ya kisasa ya upasuaji wa Ubongo iliyojengwa na Serikali ya awamu ya Tano Kwa zaidi ya Tsh Bilioni 7.9
0 comments:
Post a Comment