Saturday, 30 January 2021

Rais wa Zanzibar Dr Mwinyi Aendelea kuwasisitiza viongozi aliowateua kwenda kuwasikiliza wananchi changamoto walizonazo.

...


RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Hussein Ali Mwinyi ameendelea kuwasisitiza viongozi aliowateua kwenda kuwasikiliza wananchi changamoto walizonazo.


Alhaj Dk. Hussein Mwinyi ameyasema hayo jana wakati akitoa salamu zake kwa wananchi wa kijiji cha Nungwi mara baada ya kuungana nao katika sala ya Ijumaa huko katika Masjid Rahman iliyopo Nungwi, Wilaya ya Kaskazini A, Mkoa wa Kaskazini Unguja. 


Katika salamu zake hizo, Alhaj Dk. Mwinyi alisema kuwa kuna kila sababu kwa viongozi wake wakiwemo Wakuu wa Wilaya na Mikoa kwenda kuwasikiliza wananchi changamoto zao ili ziweze kupatiwa ufumbuzi. 


Alisema kuwa amegombea nafasi ya Urais kwa ajili ya kuwatumikia wananchi kwa kuwasikiliza matatizo yao, kero zao zikiwemo huduma za jamii kama vile afya, elimu, maji na nyenginezo ambapo hivi sasa amekuwa akifanya mikutano kadhaa na wadau wa sekta hizo kwa azma ya kutatua changamoto zilizopo.


Alisema kuwa changamoto hizo zinashughulikiwa na kusisitiza kwamba tayari alishawaambia wateule wake  wakati akiwaapisha kwamba washuke chini wakawashughulikie wananchi changamoto zao za ardhi, kuondoa dhulma na changamoto nyenginezo.


Aliwapa maagizo Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja na Mkuu wa Wilaya Kaskazini A, wakutane na uongozi kwa ajili ya kusikiliza changamoto za wananchi wa kijiji cha Nungwi na kuwataka wakatatue na yale yaliyo chini ya uwezo wao wamjuulishe ili ayafanyie utatuzi.


Alisema kuwa ana dhima ya kuhakikisha ana tenda haki kwa wananchi wote bila ya kujali uwezo wao kifedha, itikadi zao za kisiasa kwani yeye ni Rais wa Zanzibar na ana wajibu wa kuwatumikia wananchi wote bila ya kujali matabaka, rangi, dini wala kabila.



Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger