Sunday, 3 January 2021

WAZEE WASTAAFU WATEMBELEA MRADI WA UMEME WA JULIUS NYERERE...WATOA NENO KWA VIJANA

...

Mlezi wa SAWATA, Brigedia Jenerali Mstaafu Francis Xavery Mbena na wazee wenzake wakiangalia maajabu.

Na mwandishi wetu, JNHPP 
WAZEE ni hazina ya Taifa na kuna msemo wa Kiswahili usemao “Uzee ni Dawa”, Januari 2, 2021 Wazee Wastaafu kutoka Chama cha Saidia Wazee Tanzania (SAWATA) walipata fursa ya kutembelea mradi mkubwa wa kimkakati wa Umeme wa Maji wa Julius Nyerere (JNHPP 2115) unaotekelezwa kwenye bonde la mto Rufiji na kutoa neno “Vijana mlioko hapa muwe waadilifu”. 

Kilichopelekea kutolewa kwa neno hilo ni jinsi wazee hao walivyostaajabishwa na jinsi ujenzi wa bwawa hilo unavyotekelezwa kisasa tena asilimia zaidi ya 90 ni vijana wa Kitanzania ndiyo wametawala eneo hilo la kazi. 

“Tumefurahi kuwa sehemu ya mradi huu, kwa sababu hiki ni chanzo kikubwa cha kuelimisha watoto wetu, tumeona local content, watanzania wanaoshiriki katika ujenzi wa mradi huu ni wengi kwa hiyo capacity building inafanyika ipasavyo naomba tuendelee mujenga uchumi wetu na tuendelee kuijenga nchi yetu.” Alisema Balozi mstaafu Nyasugara Kadege ambaye alikuwa ni miongoni mwa wazee hao waliotembelea eneo hilo la Mradi. 

Alisema, wameelezwa faida nyingi zitokanazo na mradi huu ukiacha uzalishaji wa umeme lakini pia Mradi utadhibiti mafuriko ya mara kwa mara katika maeneo yanayozunguka mto Rufiji na pia utakuza kilimo na uvuvi. 

“Nadhani mradi huu utabadilisha maisha ya Watanzania, kwakweli tunajivunia mradi huu na tunaisifu Serikali na Tanesco kwa kusimamia mradi huu.” Alisisitiza Balozi Kadege. 

Naye mlezi wa SAWATA, Brigedia Jenerali Mstaafu Francis Xavery Mbena ameipongeza serikali ya awamu ya Tano chini ya uongozi wake Rais Dkt. John Pombe Masgufuli kwa kutekeleza mradi mkubwa kama huu ambao utaleta maendeleo makubwa katika taifa letu. 

“Tuliomba Serikalini tuje kutembelea bwaha hili la Mwalimu Nyerere ili tujifunze na kuona utaalamu wa kisasa, kitu cha kushangaza kazi hii yote nzuri imechangiwa kwa kiasi kikubwa na vijana wetu wa Kitanzania, ninachosema ni kwamba ingawa wazo la Mradi huu Mwalimu Nyerere alikuwa nalo toka zamani lakini ninaipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuutekeleza mradi.” Alisema Jenerali (Mstaafu) Mbena. 

Brigedia Jenerali (Mstaafu) Mbena aliwabeza watu wanaokejeli mradi huo na kuwaita kuwa wana mawazo ya kikoloni. “Mawazo ya Kikoloni yalikuwa kwamba Waafrika hawawezi kufanya hili au lile lakini ukweli unabaki palepale kuwa kazi hii kwa sehemu kubwa inafanywa na watu weusi w”enyewe wana uwezo wa kufanya kazi hii na tuna uwezo wa kupiga hatua katika maendeleo kama ilivyo nchi nyingine.” Alisema. 

Mzee mwingine mstaafu ni Cypriana William ambaye yeye alisema…“Tulikuwa na hamu ya kuona mradi huu, tulikuwa tunaona picha tu, lakini baada ya kufika hapa kwakweli nimeona maajabu, ninampongeza sana Rais wetu kwa kazi hii nzuri na nchi yeyu inastahili sifa, tumejifunza mengi na tunamuombea Rais baraka tele kwa Mwenyezimungu.” Alisema mzee huyo mstaafu. 

Kwa upande wake Msimamizi wa Ujenzi wa JNHPP, Mhandisi Said Kimbanga alisema Tanesco ikishirikiana na Mhandisi kutoka Tanroad watahakikisha mradi unakamilika kama ulivyopangwa. 

“Tumefikia kwenye hatua nzuri ya kuleta matumaini na wazee leo wameshuhudia kwamba kodi yao inatumika kutekeleza mradi huu na siyo pesa ya nje, na hadi sasa mradi kwa ujumla wake umefikia asilimia 40, na ni matumaini yetu ifikapo Juni 22, 2022 mradi unakamilika.” Alisema Mhandisi Kimbanga.
Msimamizi wa Ujenzi wa JNHPP, Mhandisi Said Kimbanga (kulia), akiwaonyesha kitu baadhi ya wazee hao kwenye eneo la Mradi.
Baada ya maji kuchepushwa kwenye handaki la kuchepusha maji sasa kazi inaendelea hivi.






Picha ya pamoja ya wazee wastaafu kutoka Chama Cha Saidia Wazee Tanzania (SAWATA) katika eneo la Mradi wa Umeme wa Maji wa Julius Nyerere Januari 2, 2021.
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger