Nteghenjwa Hosseah, Songwe
Naibu Waziri wa Afya Ustawi wa Jamii na Lishe Mhe. Dr. Godwin Mollel amewataka watoa huduma za Afya kuwajibika ipasavyo katika kuwahudumia wananchi.
Dr. Mollel ametoa kauli hiyo wakati akiongea na wataalamu watendaji wa Afya wa Mkoa wa Songwe katika ukumbi wa Halmashauri ya Songwe tarehe 03/01/2021.
Amesema watumishi wa Serikali kada ya Afya kuna sehemu hawawajibiki ipasavyo ndio maana malalamiko hayaishi kutoka kwa wananchi.
“Ninyi mmeajiriwa na Serikali na kila kitu kinatolewa na Serikali lakini utashangaa mtu anashindwa kutoa huduma bora
Kwa mwananchi ila mtu huyo huyo jioni unamkuta kwenye kituo binafsi anahudumia vizuri ina maana huku Serikalini anafanya makusudi kwa kutokumjali mteja? Alihoji Dr. Mollel.
Aliongeza kuwa kutokana na hali hiyo unakuta wananchi wanakimbia Kituo cha Serikali wanaenda kwenye kituo binafsi ilihali Serikalini ndio kuna wataalamu wabobezi kuliko hata huko binafsi ila kutokana na huduma zisizoridhisha mwananchi anaona bora aende akalipe hela nyingi apate huduma kuliko kutibiwa kwenye gharama nafuu hii tabia ikome kuanzia sasa na kila mmoja awajibike ipasavyo.
“ Inabidi tuanze kunyooshana pale tunaposkia malalamiko ili hadhi ya Vituo vya kutolea huduma za Afya vya Serikali irudi watu wapewe huduma bora na wafurahie huduma hizo zinazotolewa na Serikali yao hii itasaidia kuongeza mapato ya Serikali na kuendelea kuboresha huduma kwa ujumla.
Watumishi wa Afya lazima wafanye kazi kwa weledi na kufuata kanuni za maadili ya utoaji wa huduma za Afya ili kufikia malengo ya upatikanaji wa huduma bora za Afya kwa wote.
Mwisho Dr.Mollel asisitiza usimamizi makini wa miradi ya maendeleo huku akitolea mfano hospitali ya Wilaya ya Ileje inayojengwa kwa gharama ya shilingi bil 1.8 ilihali maeneo mengine wakiwa wamemaliza kiasi hicho cha fedha na ujenzi haujakamilika.
“Nizitake Halmashauri zingine ziende kujifunza Ileje ambapo wametumia bilioni 1.8 kujenga jengo zuri la Hospitali ilihali halmashauri hii iko pembezoni hata upatikanaji wa vifaa ni mgumu lakini halmashauri zingine za mjini kabisa hawajakamilisha ujenzi na fedha wamemaliza na wanaomba kuongezewa fedha nataka niwaambie tu kuwa hakuna fedha za nyongeza na hospitali hizo zikamilike” Alisema Dr Mollel.
Naye Mkurugenzi wa Huduma za Afya Ustawi wa Jamii na Lishe Dr. Ntuli Kapologwe amemshkuru Naibu Waziri wa Afya kwa maelekezo aliyoyatoa kwa watumishi watendaji wa Afya Mkoa wa Songwe na ameahidi kusimamia utekelezaji wa maagizo hayo.
Pia amewataka waganga wafawidhi wa vituo vyote vya Kutolea Huduma za Afya kuhakikisha wananunua Computer na kufunga mfumo wa GoT-HoMIS ili kudhibiti mapato ya Vituo.
0 comments:
Post a Comment