Saturday, 19 December 2020

Mume, Mke jela miaka 20 kwa kusafirisha dawa za kulevya

...


Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Rushwa na Uhujumu Uchumi maarufu kama Mahakama ya Mafisadi, imemuhukumu mfanyabiashara Ayoub Kiboko na mke wake Pilly Kiboko kifungo cha miaka 20 gerezani, baada ya kupatikana na hatia ya kusafirisha dawa za kulevya gramu 251.25 aina ya heroin.

Aidha, Mahakama hiyo imeamuru vielelezo ambavyo ni dawa za kulevya viteketezwe, huku vielelezo vingine ambavyo ni magari matatu yarudishwe kwa washtakiwa.

Hukumu hiyo imesomwa Desemba 18,2020 na Jaji Mfawidhi, Lilian Mashaka wa Mahakama hiyo, baada ya kupitia ushahidi wa mashahidi sita wa upande wa mashtaka, upande wa utetezi, vielelezo 16 na sheria na kufikia kutoa hukumu hiyo.

Jaji Mashaka amesema kuwa ushahidi wa upande wa mashtaka umethibitisha kesi kwa mshtakiwa wa kwanza (Kiboko) wa pili (Pilly) hivyo mahakama inawatia hatiani kwa makosa wanayoshitakiwa nayo ya kusafirisha dawa za kulevya.

Amesema kwa maoni yake utetezi wa washtakiwa  uliunga mkono ushahidi wa upande wa mashtaka kutokana na kujichanganya kwa maelezo yao ya ushahidi waliyoutoa Mahakamani hapo.

Mahakama imezingatia sheria za dawa za kulevya na pia tangu washtakiwa wakamatwe Mei 23, 2018 na muda wote, waliokaa gerezani, hivyo imewahukumu kifungo cha miaka 20 jela na kama hawajaridhika wana haki ya kukata rufaa.


Baada ya washtakiwa kutiwa hatiani, Jaji Mashaka aliwauliza kama wanachochote cha kusema, ambapo Kiboko aliiomba mahakama isiwape adhabu kali licha ya kutiwa hatiani na pia ni shtaka la kwanza kutenda.

Kwa upande wa Pilly, aliiomba mahakama imuhurumie kwa sababu ana watoto watatu, hajawaona kwa muda mrefu, hivyo mahakama imuonee huruma.



Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger