Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila amemhakikishia aliyekuwa mbunge wa Mbeya Mjini kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Joseph Mbilinyi maarufu kama ‘Sugu’, kuwa hoteli yake inayodaiwa kujengwa kwenye chanzo cha maji haitobomolewa.
Katika siku za karibu kulikuwa na uvumi kwamba hoteli hiyo itabomolewa kwa sababu ipo kwenye chanzo cha maji lakini leo, Chalamila ameeleza kuwa Rais John Magufuli amemtuma aeleze kwamba mtu yeyote hatakiwi kusema anabomoa hoteli hiyo.
“Kwa sababu huyu ni mwekezaji kama wawekezaji wengine na ikiwezekana amedai kama tuna viwanja vingine upande huu wa Uzunguni basi moja ya watu wanaotakiwa kufaidika navyo ni pamoja na Sugu ambaye amekwishaanza kuwekeza hapa.
“Hoteli hii ilianza kupimwa ardhi maana yake ardhi hii imepimwa na ina hati, watu wa mipango miji na wanaohusika na upimaji walishapima maana yake hadi mkurugenzi wa ramani anafahamu eneo, sasa kama umetoa hati kwenye eneo lenye chanzo cha maji na leo unategemea baada ya kusimika hoteli ulitaka iweje, kwa hiyo vibali vyote vilifuatwa mlolongo wake,” amesema Chalamila.
Ameongeza, “Mmeona anatunza maji vizuri na maji yanatirika vizuri na hayajakauka. Inawezekana hoteli nyingine ambazo zimekausha maji sio hii, suala hili lisipelekee mvurugano wa kisiasa, mimi kauli yangu nasema maji ataendelea kuyatunza kama mnavyoona.
“Hoteli hii watu wa NEMC wanaijua, watu wa OSHA wanaijua, watu wa halmashauri wanaijua, mkuu wa mkoa anaijua, TRA wanaijua sasa kama wote tunaijua leo iweje tuseme iko kwenye maji, wakati inajengwa walikuwa wapi, wakati tunapima ardhi ilikuwa wapi au mto haukuwepo umekuja le?.”
Sugu amesema kuwa anaamini ujumbe uliobebwa kwenye salamu za rais utasaidia kuleta kujiamini hata kwa wafanyabiashara wengine, kama itatokea nafasi ya kuwekeza zaidi Mbeya.
0 comments:
Post a Comment