Askari wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Koplo Denis Minja, ambaye mwezi Mei alimwokoa mtoto mchanga akiwa hai ndani ya shimo la choo wilayani Ngara mkoani Kagera, amemwokoa tena mtoto mwingine wa kiume mwenye umri wa miaka 2, kutoka katika shimo la choo, eneo la Kayanga wilayani Karagwe.
Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji mkoani Kagera, Hamis Dawa, amesema kuwa walipata taarifa za mtoto kutumbukia katika choo cha shimo wakati akimfuata mama yake aliyekuwa bafuni akioga na kwenda kumuokoa na kufanikiwa kumtoa akiwa hai na kwa sasa anaendelea vizuri.
Amesema Askari huyo Koplo Minja, ambaye alishirikiana na Askari wenzake na kuingia katika shimo hilo kumwokoa mtoto huyo, kituo chake cha kazi ni wilaya ya Ngara lakini yuko wilayani Karagwe kumuuguza mke wake.
Dawa amesema kuwa tukio hilo limetokea Desemba 28 mwaka huu, saa 10:00 jioni, na kutaja Askari wengine wa zimamoto walioshiriki kuokoa maisha ya mtoto huyo kuwa ni Norbert Saka, Eliad Batanyangwa na James Lucas.
Aidha Mkuu huyo wa Zimamoto na Uokoaji ametumia fursa hiyo kuwaasa wazazi kuacha tabia ya kwenda na watoto wadogo katika maeneo hatarishi ikiwamo chooni na mtoni, ili kuepusha majanga kama hayo na kuwa uchunguzi wa kina unaendelea.
0 comments:
Post a Comment