Na Dotto Mwaibale.
KANISA la Abundant Blessing Centre (ABC) la Mtaa wa Mandela jijini Dar es Salaam limetoa msaada wa chakula na vitu vingine kwa ajili ya kuwasaidia Wagane na Wajane 50 wanaoishi kwenye mtaa huo.
Mbali na kutoa msaada pia kanisa hilo limetoa msaada wa vifaa vya shuleni kama madaftari na kalamu kwa watoto 20 wenye uhitaji ikiwa ni maandalizi ya masomo watakayoanza Januari 2021.
Akizungumza juzi wakati wa kukabidhi msaada huo Askofu Kiongozi wa kanisa hilo Flaston Ndabila alisema wamekuwa wakiguswa na changamoto mbalimbali za Wajane na wagane pamoja na wanafunzi wanaoishi mtaa huo na ndio maana kama kanisa wameweka utaratibu kila mwaka kutoa msaada huo.
"Huu ni mwaka wetu wa tano tumekuwa tukifanya hivi hasa kipindi hiki cha Sikukuu za mwishoni mwa mwaka za Krismas na mwaka mpya kuelekea mwezi wa kwanza ambapo watoto hawa wenye uhitaji wanakuwa wanakabiliwa na changamoto ya vifaa vya shule" alisema Ndabila.
Aidha Ndabila alisema wanatoa msaada huo kwa wanafunzi hao ikiwa ni kuunga mkono jitihada za Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dkt.John Magufuli ambayo inatoa elimu bure kuanzia shule ya msingi hadi sekondari.
Wajumbe wa Serikali ya mtaa wa Mandela, Leonard Chalema na Tabrisa Bushiri kwa niaba ya Mwenyekiti wa mtaa huo, Yusufu Nyumbi wakipokea msaada huo wamelishukuru kanisa hilo kwa utaratibu wao wa kila mwaka wa kuwajali wenye uhitaji.
Mgane Hussein Libe ambaye huu ni mwaka wake wa tatu kupata msaada huo alisema kanisa hilo ni mfano wa kuigwa na akashauri makanisa mengine kuiga mfano huo wa kusaidia jamii badala ya kuiachia Serikali pekee kufanya hivyo.
Hosiana Mkono ambaye ni mjane amelishukuru kanisa hilo kwa kutoa msaada huo na kugusa maisha ya wenye uhitaji.
0 comments:
Post a Comment