Wednesday, 30 December 2020

Waziri Mkuu Amuwakilisha Rais Dkt. Magufuli Mazishi Ya Askofu Banzi

...


 *Awataka Watanzania wamuenzi kwa kuuishi utumishi wake
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametoa wito kwa Watanzania kumuenzi Askofu Mkuu wa Jimbo Katoliki la Tanga, Baba Askofu Anthony Mathias Banzi kwa kuuishi utumishi wake uliogubikwa na upole na unyenyekevu aliowaonesha wakati wa kipindi cha uchungaji wake.

Ametoa wito huo leo (Jumanne, Desemba 29, 2020) kwenye mazishi ya Askofu Banzi yaliyofanyika ndani ya Kanisa Kuu la Mtakatifu Anthony wa Padua, Jimbo Katoliki la Tanga. Waziri Mkuu ameshiriki mazishi hayo kwa niaba ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli. Ibada ya mazishi imeongozwa na Askofu Mkuu wa Jimbo Katoliki la Mtwara, Askofu Titus Mdoe.

Waziri Mkuu amesema katika maisha na utume wake wa kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu, Askofu Banzi alitoa kipaumbele katika masuala mbalimbali ya kijamii zikiwemo za elimu, afya na maji. Askofu Banzi alifariki dunia Jumapili, Desemba 20, 2020 katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, jijini Dar es Salaam alikokuwa akipatiwa matibabu.

“Leo hii tunapomsindikiza Baba Askofu Anthony Banzi tunajivunia mchango wake mkubwa katika kupigania amani, maelewano na mtangamano wa jamii kwa lengo la kujenga umoja, upendo na mshikamano wa Kitanzania. Sisi upande wa Serikali tutamkumbuka sana.”

Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kutoa pole kwa familia, ndugu na jamaa, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania na waamini wote wa kikatoliki nchini. “Tumuombee kwa Mwenyezi Mungu azipokee kazi zake za kiuchungaji alizozifanya katika kipindi cha uhai wake na ampumzishe kwa amani.”

Naye, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Ummy Mwalimu amesema kuwa wanawake wa Mkoa wa Tanga wamempoteza baba mwema na mlezi ambaye alipenda kuwashauri na kuwaunganisha kama watoto wake kwa kutumia kaulimbiu yake ya hekima, umoja na amani

“Mimi ni mmoja wa wanufaika wa upendo, wema na hekima za baba Askofu, licha ya kuwa mimi sio Mkatoliki lakini baba Askofu Banzi amekuwa akinikaribisha nyumbani kwake na kunipa baraka zake na kuniombea kwa sababu yeye anaamini watu wote ni wamoja”

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martine Shigela amesema Baba askofu Banzi alikuwa ni kiongozi mnyenyekevu, muadilifu na mpenda maendeleo aliyependa kuuona mkoa wa Tanga unapiga hatua.

Akisoma wasifu wa marehemu Askofu Banzi, Padri Richard Kimbwi alisema alizaliwa Oktoba 28, 1946 katika Parokia ya Tawa, Jimbo Katoliki la Morogoro, ambapo baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, Julai 29, 1973 alipewa daraja takatifu la upadre, Jimbo Katoliki la Morogoro.

Alisema kuwa Mwaka 1976 aliteulia kuwa Msarifu wa Seminari kuu ya Ntungano, Jimbo Katoliki la Bukoba na mwaka 1976 hadi mwaka 1981 alipelekwa nchini Austria kwa masomo ya juu na kufanikiwa kutunukiwa Shahada ya Uzamivu katika Falsafa. Mwaka 1981 hadi mwaka 1982 aliteuliwa kuwa Paroko wa Parokia ya Mandera na mhudumu wa maisha kiroho kwenye Hospitali ya Turiani, Jimbo Katoliki la Morogoro.

Aidha, mwaka 1981 hadi mwaka 1985 aliteuliwa kuwa Mhasibu wa Jimbo Katoliki la Morogoro na kati ya Mwaka 1985 hadi mwaka 1987 alikuwa ni Padre wa kiroho, Sekondari ya Masista Bigwa, Morogoro. Kati ya Mwaka 1988 hadi mwaka 1991 alikuwa mwalimu na mlezi, Seminari kuu ya Ntungano, Jimbo Katoliki la Bukoba na baadaye akateuliwa kuwa Gambera.

Mwaka 1992 hadi mwaka 1994 aliteuliwa kuwa Gambera wa Seminari kuu ya Kibosho, Jimbo Katoliki la Moshi na ilipofika tarehe 10 Juni 1994, Mtakatifu Yohane Paulo II akamteuwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki Tanga na kuwekwa wakfu tarehe 15 Septemba 1994 na Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mstaafu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam.

Alisema Askofu Banzi amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 74 ya kuzaliwa, miaka 47 ya Daraja Takatifu la Upadre na miaka 26 ya Uaskofu, Utume ambao aliufanya kwa uaminifu mkubwa katika kuwaongoza, kuwafundisha na kuwatakatifuza watu wa Mungu ndani na nje ya Jimbo Katoliki la Tanga.


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger