Sunday, 27 December 2020

Msajili Baraza La Famasi Avitaka Vyuo Vya Kada Ya Famasi Kuzingatia Vigezo Vya Mafunzo

...


 Na. Catherine Sungura,WAMJW-Dodoma
Wamiliki wa vyuo binafsi vya kada ya famasi nchini wametakiwa wasibadilishe vyuo vikawa kama biashara kwani Serikali inatarajia kupata wataalam ambao wataweza kutoa huduma zinazostahili kwenye vituo vya kutolea huduma za afya nchini.

Wito huo umetolewa hivi karibuni na Msajili wa Baraza la Famasi Bi. Elizabeth Shekalaghe ofisini kwake jijini Dodoma.

Bi. Shekalaghe alisema kuwa kila mwaka idadi ya vyuo inaongezeka na hadi sasa Baraza limeidhinisha vyuo 52 ngazi ya cheti hadi diploma ambavyo tayari vimesajiliwa na NACTE hivyo lazima kuwe na aina ya wataalam wenye uwezo ambao wanaendana na mahitaji ya sasa.

“Kama Baraza la Famasi tunao wajibu wa kusimamia kwa umakini vyuo ili kuhakikisha ubora wa mafunzo yatolewayo iendane na mitaala na mahitaji kulingana na hali ya sasa”.Alisema

Aidha, Msajili huyo alisema idadi ya wataalam hao nchini imekua ikiongezeka japo si kwa kasi kubwa na kuongeza kuwa kwa kipindi cha mwaka 2018/2019 walisajili wafamasia 174 na mwaka 2019/2020 wafamasia 219 walisajiliwa na kupelekea kuwa na wafamasia 2111 nchini.

Kwa upande wa fundi dawa sanifu kwa miaka miwili iliyopita Bi. Shekalaghe alisema waliweza kusajili wataalam hao 365 na hivyo kuwa na mafundi dawa sanifu 3040 hapa nchini.

“Upande wa fundi dawa sanifu kwa mwaka huu tumesajili wapatao 694,kada hii bado inahitajika ili kuweza kusimamia utoaji wa dawa kwenye vituo licha ya kwamba bado wanaendelea na mafunzo ngazi ya stashahada”.

Kwa upande wa usimamizi wa maduka ya dawa muhimu, Msajili huyo alisema baraza la famasi limekasimu baadhi ya majukumu katika ngazi ya halmashauri kwa mujibu wa sheria hivyo wameendelea kuendesha mafunzo kwa wakaguzi ili kuwakumbusha maadili,miiko na majukumu yao kama wafamasia na wakaguzi.

Bi. Shekalaghe,alisema kwa mwaka mpya ujao wamejipanga kumalizia kuwajengea uwezo wakaguzi hao nchi nzima na suala hili litakua endelevu. Amewakumbusha wananchi kutojinunulia dawa kiholela kwa kuwa inaweza kuwasababishia madhara kiafya na hivyo ni vema wakafanya vipimo ili kupata tiba sahihi.


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger