Thursday, 31 December 2020

VITA DHIDI YA UKEKETAJI YALETA MAFANIKIO SINGIDA

...

Baadhi ya vifaa vinavyotumika kwenye Ukeketaji vikisalimishwa na Ngariba aliyetangaza kuachana kazi hiyo
Mmoja wa Wadau wa kupinga vitendo vya  Ukeketaji, Patrick Kasango  akitoa elimu kwa wananchi

Na Abby Nkungu, Singida


VITA dhidi ya ukeketaji wanawake na watoto wa kike imeanza kuonesha mafanikio mkoani Singida baada ya wazazi na walezi wa kike waliokuwa wanatajwa kuwa kikwazo kikubwa katika suala hilo, kuanza kujitokeza hadharani kupinga mila hiyo potofu yenye madhara makubwa kiafya.

 

Awali, ilielezwa kuwa licha ya juhudi kubwa za Serikali na Mashirika mbalimbali kudumisha usalama na ulinzi wa mtoto kwa kuzuia mila hiyo potofu, wazazi na walezi wa kike waliendelea kuwa kikwazo kwa kubuni mbinu mpya ya ukeketaji watoto wachanga kwa siri ili kukwepa mkono wa sheria.

 

Ilielezwa kuwa baada ya Serikali kutunga Sheria inayotaja ukeketaji kuwa kosa la jinai, baadhi ya wazazi na walezi wa kike walikuja na mbinu mpya ya kufanya kitendo hicho kiovu na cha kikatili kwa siri usiku wa manane kwa kumsugua mtoto mchanga sehemu zake za siri kwa majivu au chumvi aina ya magadi hadi damu itoke au kukata kwa kucha sehemu hiyo ili kutekeleza mila hiyo potofu.

 

Hata hivyo, Mratibu wa Shirika la ESTL linalotekeleza Mradi wa kupinga ukatili wa kijinsia katika Wilaya ya Singida, Filbert Swai anasema baada ya elimu kutolewa kwa wingi, yapo mafanikio yaliyoanza kujitokeza kama vile baadhi ya  ngariba, wazazi na walezi wa kike kuanza kupinga mila hiyo hadharani.

 

“Ikiwa wazazi wa kike na baadhi ya ngariba ambao ndio walikuwa vinara wa kufanya jambo hilo kwa siri usiku wa manane, sasa wameanza kujitokeza mchana kweupe na  kutangaza  kupinga mila hiyo kwenye mikutano ya hadhara ni dhahiri kuwa vita hii tunaenda kushinda” alisema na kuongeza;

 

Pamoja na kudumisha mila,  wengi walishindwa kuacha vitendo hivyo kutokana na dhana potofu kuwa ukeketaji ni tiba ya ugonjwa unaojulikana kienyeji kama 'lawawala'. Baada ya kutumia waatalamu wa afya kutoa elimu kuwa 'lawalawa' inaweza kuzuiwa kwa kuimarisha usafi sehemu za siri za mtoto, baadhi yao wameacha".

 

Ngariba mstaafu, Halima Ntandu (76) Mkazi wa Ntuntu wilayani Ikungi alisema yeye ameacha kabisa kufanya ukeketaji baada ya kupata elimu kupitia vyombo vya  habari na mikutano ya hadhara juu ya madhara ya ukeketaji na hatua zinazoweza kuchukuliwa iwapo mtu atabainika kukeketa.

 

“Tulianza kufanya usiku wa manane lakini nikaja kuambiwa na wajukuu wangu kuwa bibi wameandika hadi kwenye magazeti kuwa mmebadili mbinu, nikasema yuuu nisije kikafungwa bure  na uzee huu, nikaacha kabisa!!” anasema bibi huyo na kutoa mwito kwa ngariba wenzake kustaafu kwa hiari. 

 

 

Daktari Bingwa Mshauri wa magonjwa ya Wanawake na Watoto katika Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Singida,  Dk Suleiman Muttani alipohojiwa alisema ingawa mila hiyo imeanza kupungua, bado ni kikwazo cha ulinzi na usalama wa mtoto mkoani Singida kutokana na athari za kiafya na kisaikosojia zinazomkuta mhusika ikiwa ni pamoja na athari za  muda mrefu na muda mfupi.

 

"Athari hizo ni kutokwa na damu nyingi sehemu za siri au wakati mwingine kusababisha kifo na maambukizi ya magonjwa ya Ukimwi na mengine. Magonjwa ya kuambukiza ya mara kwa mara yanayoweza kumfanya mtoto kuwa tasa anapofikia ukubwani, uharibifu wa mfumo wa njia ya uzazi, matatizo wakati wa kujifungua na kutofurahia tendo la ndoa wakati wa kujamiana kutokana na kovu linalobaki baada ya majeraha kupona" alifafanua Dk Muttani.

 

Kwa mujibu wa takwimu za utafiti wa Kidemografia na Afya (TDHS), kiwango cha ukeketaji wanawake wenye umri wa miaka 15 - 49 kimekupungua kutoka asilimia 18 mwaka 1996 hadi kufikia asilimia 10 mwaka 2016. 

Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger