Friday, 13 November 2020

Serikali Itahakikisha Wakulima Wa Miwa Wanapata Soko La Uhakika-Kusaya.

...


Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya amekitaka kiwanda cha sukari Kilombero kuongeza wigo wa ununuzi wa miwa ya wakulima ili uzalishaji wa sukari nchini uongezeke na kuondoa utegemezi wa sukari toka nje ya nchi.


Katibu Mkuu huyo ametoa agizo hilo leo (12.11.2020) wilayani Kilombero  wakati akifungua Maonesho ya Siku ya Wakulima wa Miwa yaliyoandaliwa na wadau wa sekta ya sukari nchini.


“Kiwanda cha Sukari Kilombero hakikisheni mkakati wenu wa kuongeza uwezo wa kiwanda kuzalisha sukari toka tani 120,000 za sasa hadi tani 160,000 kwa mwaka unakamilika mapema ili miwa ya wakulima isikose soko kuchakatwa ” aliagiza Kusaya.

Kusaya alisema hayo kufuatia risala ya wakulima wa miwa wa Kilombero kuonesha kuwa uwezo wa kiwanda cha Kilombero kwa sasa ni kuchakata miwa tani 600,000 wakati uzalishaji toka kwa wakulima wadogo kwenye vyama vya msingi 20 vilivyopo Bonde la Kilombero umefikia tani 900,000 kwa mwaka hali inayopelekea malalamiko ya miwa kutonunuliwa.

Katibu Mkuu huyo wa wizara ya Kilimo alisema hali ya uzalishaji sukari nchini bado ni mdogo kukidhi mahitaji ya soko la ndani ambalo ni tani 450,000 kwa mwaka wakati uzalishaji wa viwanda vyote umefikia tani 350,000 hivyo kufanya nchi kutokuwa na utoshelevu wa sukari.

Kiwanda cha Sukari Kilombero kinaongoza nchini kwa kuzalisha sukari asilimia 65 inayochangiwa na wakulima wadogo kwa asilimia 30 toka wilaya za Kilombero na Kilosa hivyo serikali kwa kushirikiana na kiwanda hicho wataendelea kuweka mazingira wezeshi ya kupanua kiwanda.

Ili kukabiliana na upungufu wa sukari nchini Kusaya alisema serikali imeanzisha shamba la miwa Mkulazi ambapo itajenga kiwanda kikubwa cha sukari chenye uwezo wa kuzalisha tani 200,000 kwa mwaka na kuwa inaendelea pia kuhamasisha wawekezaji wengi zaidi kuanzisha viwanda vya sukari nchini

Katika hatua nyingine, Kusaya ametoa rai kwa taasisi za fedha ikiwemo mabenki ya biashara nchini kutoa mikopo yenye masharti nafuu ili wakulima wengi zaidi waweze kuanzisha mashamba ya miwa na viwanda vidogo vidogo vya sukari kukabiliana na changamoto ya mara kwa mara ya nchi kukosa sukari.

Kusaya alizitaka taasisi za fedha ikiwemo benki za NMB na CRDB kuangalia namna ya kupunguza riba kwa mikopo ya wakulima ili wasione ni mizigo na kushindwa kuwekeza kwenye sekta ya kilimo.

“ Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dkt.John John Pombe Magufuli tunataka kutimiza malengo ya msingi ya kuhakikisha tunatengeneza mabilionea wengi zaidi kutokana na uwekezaji kwenye kilimo“ alisisitiza Kusaya

Akizungumza na wakulima wa miwa na wadau wa sukari waliokusanyika Kilombero ,Kusaya amesema lengo la maonesho hayo ni kuhamasisha uzalishaji miwa unaotumia teknolojia ya kisasa na matumizi ya mbegu bora ili kuwezesha nchi kuwa na utoshelevu wa sukari.


Akizungumza kwenye maonesho hayo Afisa Ushirika na Msimamizi wa wakulima wa Bonde la Kilombero  Jackson Mushumba alisema changamoto iliyopo sasa ni kiwanda cha sukari kuchukua miwa kigodo tofauti ya inayozalishwa na wakulima hali inayopelekea malalamiko na hasara.


"Wakulima wadogo wanazalisha miwa tani 900,000 kwa mwaka wakati uwezo kiwanda ni kuchakata miwa tani 600,000 tu kwa mwaka hivyo kuhitaji viwanda zaidi" alisema Mushumba.


Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu Kiwanda cha Sukari Kilombero Guy Williams alisema wapo kwenye mkakati wa kupanua uwezo wa kiwanda ili changamoto ya miwa ya wakulima imalizike .


Williams aliongeza kusema kuwa kiwanda hicho kinaishi kwenye mwanga na maelekezo ya Rais Dkt.John Pombe Magufuli kuhakikisha kinapanuka na kuwa ifikapo mwakani wamiliki na wenye hisa wawili wakubwa watakamilisha makubaliano ili kiwanda cha kisasa kianzishwe na kuchukua miwa yote ya wakulima.


"COVID- 19 ilituweka chini lakini sasa tumejipanga kurudia mazungumzo na makubaliano ili ifikapo Aprili 2021 tutaweza kupanua uwezo wa kiwanda kuchukua miwa yote ya wakulima takribani tani 800,000" alisema Williams.


Naye Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro Mhandisi Emmanuel Klobero akitoa salamu za mkoa kwenye maonesho hayo aliwapongeza wakulima wa miwa wa Kilombero na Kilosa kwa kazi nzuri ya uzalishaji hai inayoufanya mkoa wa huo kuongoza nchini kwa uzalishaji wa sukari.

Mhandisi Kalobero aliongeza kusema wanatambua changamoto za wakulima wa miwa ikiwemo tatizo la uchomaji moto mashamba na uwepo wa wadudu wasumbufu waitwao vidung’ata wa njano wanoshambulia miwa shambani hali inayowapunguzia kipato wakulima na kuwa serikali kupitia Kituo cha utafiti wa Kilimo (TARI) unashugulikia changamoto hizo haraka.

 Maonesho hayo yameshirikisha wadau ikiwemo kiwanda cha sukari Kilombero, Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI),Bodi ya Sukari, Taasisi za fedha, Chuo cha Taifa cha Sukari na wakulima toka Wilaya za Kilombero na Kilosa.


Mwisho
Imeandaliwa na;
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Kilimo
KILOMBERO
12.11.2020




Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger