Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maridhiano Tanzania, Sheikh Alhad Mussa akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dodoma, kumshukuru Mungu kwa Uchaguzi Mkuu wa Tanzania kufanyika kwa amani na utulivu. Kushoto ni Katibu Mkuu wa Jumuia hiyo, Askofu Oswald Mlay na Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo Mkoa wa Dodoma, Askofu Evance Chande. PICHA NA RICHARD MWAIKENDA
Na Richard Mwaikenda, CCM Blog, Dodoma.
MWENYEKITI wa Tume ya Maridhiano Tanzania, Sheikh Alhad Mussa Salumu amewasihi watanzania kuendelea kumshukuru Mungu kwa wema aliowatendea baada ya Uchaguzi Mkuu wa Tanzania kufanyika kwa salama na amani.
Ameyazungumza hayo wakati wa mkutano na waandishi wa habari jijini Dodoma leo, akiwa pamoja na wajumbe wa tume ya kitaifa ya maridhiano na wa mkoa wa Dodoma.
Aidha, Sheikh Alhad Mussa amesema kuwa inatakiwa sasa baada ya uchaguzi kumalizika salama ni kuungana kuendelea kuiombea kwa Mungu serikali iliyoshinda iongoze vema.
"Tunashukuru Mungu Uchaguzi umeisha kwa amani na salama, kilicho mbele yetu ni kuungana kuendelea kuiombea Mungu Serikali iliyopo madarakani ituongoze salama.
Katika chaguzi zote kuna kushinda na kushindwa, huwezi kukubalika na kila mmoja haiwezekani, manabii wa Mwenyezi Mungu na hata Wacha Mungu hawakukubalika nao walipingwa, hii ni desturi ni jambo la kawaida,"amesema Sheikh Alhad.
Ameshauri upande ambao haujaridhika usisababishe vurugu, bali ufuate taratibu zilizopo ikiwemo ya kisheria na hata jumuiya hiyo inaweza kuweka mambo sawa.
"Kubwa tunawaomba Watanzania Nchi yetu iendelee kuwa salama na utulivu, tunahitaji nchi yenye amani ili tuweze kufanya shughuli zetu kwa ukamilifu bila bughudha yoyote, tusijaribu kuchezea amani iliyopo, tutajuta, tuna mifano mingi ya nchi mbalimbali zilizochezea amani, kuirejesha ni ngumu sana."
Amesema viongozi wa Dini walimlilia sana Mungu ili Uchaguzi uvuke kwa salama na amani, hivyo inabidi kumshukuru Mungu kwa wema wake aliotutendea. na kwamba wakifanya hivyo Mungu atatuzidishia.
Alimalizia kwa kutoa shukrani kwa viongozi wote walioiombea kwa Mungu nchi wakati wa mlipuko wa ugonjwa wa corona na Uchaguzi Mkuu na sasa iko salama hivyo tuendelee kumshukuru Mungu naye ataendelea kutusikiliza.
0 comments:
Post a Comment