Rais Donald Trump amedai kushinda uchaguzi wa Marekani licha ya kwamba matokeo ya mwisho bado hayajatangazwa, na amesema atakwenda Mahakama ya Juu kupinga kuendelea kuhesabiwa kwa kura.
Trump amedai ushindi huo katika hotuba isiyo ya kawaida akiwa ikulu ya White House, na kuongeza kuwa kuendelea kuhesabiwa kwa kura ni njama ya kufanya udanganyifu.
Mrepublican huyo ambaye matokeo ya awali yanamuonesha akiwa katika mchuano mkali na Mdemocrat Joe Biden, amesema atakwenda mahakamani na anataka upigaji kura wote kusimama - akionekana kumaanisha kusitisha kuhesabiwa kwa kura za posta, ambako kunaweza kuruhusiwa kisheria na bodi za uchaguzi za majimbo baada ya uchaguzi wa Jumanne iwapo zilikuja kwa wakati.
Suala hilo linaweza kugeuka nyeti katika majimbo ambayo yanaendelea kuhesabu kura katika kinyang'anyiro hicho kikali.
Timu ya kampeni ya Joe Biden imekosoa matamshi hayo ya Trump na kuyataja kuwa kashfa, na baadhi ya wanachama wa chama chake cha Repulican pia wameikosoa hatua hiyo.
0 comments:
Post a Comment