TAASISI
ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) leo tarehe 1/4/2016
imewafikisha Mahakamani aliyekuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato
Tanzania na Mwenyekiti wa ‘Enterprise Growth Market Advisors Ltd’ (EGMA),
Bw. Harry Msamire Kitilya; aliyekuwa Mkuu wa Idara ya Ushirikiano na
Uwekezaji wa Benki ya Stanbic Tanzania, Shose Mori Sinare pamoja na
Aliyekuwa Mwanasheria wa Benki ya Stanbic Tanzania, Bw. Sioi Graham
Solomon.
Washtakiwa
wote wanashtakiwa kwa makosa ya:- Kula njama na kujipatia kwa
udanganyifu kinyume na kifungu Na. 384 cha Kanuni ya Adhabu (Cap 16
R.E. 2002) ; Kughushi kinyume na kifungu Na. 333,335 (a) na 337 cha
Kanuni ya Adhabu (Cap 16 R.E 2002) ; Utakatishaji wa fedha haramu
kinyume na kifungu Na. 12 (a) 13 (a) cha Sheria ya ya Utakatishaji fedha
Na. 12 ya Mwaka 2006 ‘Anti- Money Laundering Act’.
Mashtaka
hayo yalisomwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Mhe.
Hakimu Emirius Mchauro. Kwa upande wa Jamhuri kesi hii inasimamiwa na
Mwendesha Mashtaka Mwandamizi wa Serikali Herman Tibabyekomia,
Christopher Msigwa na Mwendesha Mastaka wa TAKUKURU Stanley Luoga.
Washtakiwa wanatetewa na Wakili wa Kujitegemea Ringo Tenga, Rosai
Mbwambo, Semo na Nyaisa.
Washitakiwa
wote watatu wamepelekwa rumande, wamekosa dhamana kwani Kifungu Na.
148 (5) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA) Kinazuia utoaji
wa dhamana kwa washtakiwa wa Utakatishaji wa fedha haramu. Kesi hii
itatajwa tena tarehe 8/4/2016.
IMETOLEWA NA
OFISI YA AFISA UHUSIANO
TAASISI YA KUZUIA NA KUPAMBANA NA RUSHWA, MAKAO MAKUU
1 APRIL, 2016.
0 comments:
Post a Comment