OWM-TAMISEMI.
OWM-TAMISEMI kwa kushirikiana na
Taasisi ya Elimu
Tanzania (TET) imeandaa mafunzo kwa Walimu wa Shule za Msingi kwa lengo
la kuwajengea uwezo wa kufundisha Mtaala mpya wa Elimu ya Msingi Darasa
la I na la II. Mtaala huu unatokana na malengo ya Serikali ya kukuza
stadi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK). Mafunzo haya pia yatatolewa
kwa Walimu ambao watawezesha ufundishaji na ujifunzaji wa KKK kwa
watoto walio katika vituo vya Elimu nje ya Mfumo Rasmi
Mafunzo
hayo yamepangwa kufanyika katika awamu nne katika Chuo Kikuu cha
Dodoma. Awamu ya kwanza itaanza tarehe 13 hadi 21 Aprili 2015; Awamu ya
pili tarehe 27 Aprili hadi 6 Mei, 2015; awamu ya tatu tarehe 11 hadi 20
Mei, 2015; na awamu ya nne itakuwa tarehe 25 Mei hadi tarehe 3 Juni,
2015.
Walimu 4,430 kutoka mikoa ya Arusha, Dar es
Salaam, Tanga, Singida, Rukwa, Ruvuma, Morogoro na Pwani watashiriki
mafunzo katika awamu ya kwanza. Walimu 4,492 watashiriki mafunzo katika
awamu ya pili kutoka mikoa ya Kilimanjaro, Manyara, Simiyu, Katavi,
Geita, na Mwanza. Aidha, walimu 9,078 watashiriki katika awamu ya tatu
na ya nne ya mafunzo hayo.
Hivyo, jumla ya walimu
18,000 kutoka mikoa 14 wanatarajiwa kushiriki mafunzo hayo chini ya
mpango wa Serikali unaofadhiliwa na Ushirika wa Kimataifa wa Maendeleo
ya Elimu, (Global Partnership for Education-GPE).
Aidha
walimu kutoka katika mikoa 11 watapatiwa mafunzo chini ya mipango ya
wahisani tofauti, ambapo walimu wa mkoa wa Mtwara walishapatiwa mafunzo
hayo chini ya Shirika la Maendeleo la Marekani –USAID; Mikoa ya
Kigoma, Tabora, Lindi, Simiyu, Mara, Shinyanga na Dodoma wanaendelea
kupatiwa mafunzo chini ya ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Uingereza-
DfID na mikoa ya Mbeya, Njombe, na Iringa watapata mafunzo chini ya
ufadhili wa Shirika Watoto la Umoja wa Mataifa- UNICEF.
Imetolewa na Jumanne A. Sagini ( Katibu Mkuu -OWM-TAMISEMI ).
0 comments:
Post a Comment