Wednesday, 16 April 2025

WANANCHI KYERWA WAMPONGEZA RAIS SAMIA KUWALETEA MSAADA WA KISHERIA

...
Na Lydia Lugakila -Kyerwa

Wananchi katika Halmashauri ya wilaya ya Kyerwa Mkoani Kagera ya wilaya ya kyerwa wamemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwasogea karibu huduma ya msaada wa kisheria kupitia kampeini ya msaada wa kisheria ya Mama Samia ijulikanayo kama Samia Legal Aid Campaign kwani imemulika migogoro mingi ikiwemo ya ndoa na ya ardhi.

Kauli hiyo imetolewa na  baadhi ya Wananchi katika kijiji cha kibimba kata ya Mabira waliojitokeza katika kampeini hiyo.

 Philbat France na Mathayo Bernard wemesema kuwa kuwepo kwa ujio wa kampeini hiyo katika ngazi ya vijijini inaenda kuwa mkombozi kwani familia nyingi zipo katika hali mbaya juu ya migogoro ikiwemo ya ndoa huku wakimtaja Rais Samia kuwa Mkombozi wao.

Aidha wameongeza kuwa familia nyingi zimekuwa na changamoto ya migogoro ya ndoa inayosababishwa na watoto wao wenyewe ambayo mwisho wa siku inasababisha migogoro ya ardhi mpaka kusababisha kufanyiana vitendo vibaya wakati mwingine, kwani asilimia kubwa ya waathirika katika mgogoro hiyo ni wanaume hasa pale wanapopigwa na wake zao .

Pia wamesema kupitia uelewa walioupata kutoka kwa Wataalam hao itasaidia kukuza malezi bora ya familia zao hasa kwa watoto na kuwa na uelewa juu ya mirathi katika familia zao.

Naye Getruda Mwiga kutoka dawati la jinsia na watoto ambaye naye ni miongoni mwa timu ya kampeini ya msaada wa kisheria ya Mama Samia ambapo amewasihi wazazi kudumisha malezi bora kwa watoto wao kwani hiyo itasaidia kuondoa changamoto hizo katika jamii.

“Malezi bora kwa watoto wetu ni muhimu pia kama familia tunatakiwa kusikiliza na unapopata changamoto usisite kutoa taarifa ili kupata msaada mfano kwa wakina Baba najua mnakutana na changamoto nyingi huko katika makazi yenu ila msiwe na aibu kutoa taarifa kwani itawasaidia kutojichukulia sheria mkononi”

Kwa upande wake afisa ardhi mwandamizi Bw. Bitabonwa Mkama amesema kila mwananchi anayo haki ya kumiliki ardhi kisheria bila kubagua jinsia na kupitia kampeini hiyo ya msaada wa kisheria itakuwa ni fursa kupata msaada zaidi.

Sambamba na hayo pia  Bitabonwa katika kutoa elimu hiyo ya msaada wa kisheria juu ya umiliki wa ardhi amekutana na changamoto ya kutokuwepo kwa mabaraza ya ardhi ya vijiji jambo linalopelekea migogoro mingi ya ardhi katika vijiji hivyo ambapo ameahidi jambo hilo kufanyiwa kazi kupitia kampeini hiyo.


Share:

Related Posts:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © 2025 MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger