Monday, 7 April 2025

MKOA WA LINDI WAKO TAYARI KUUPOKEA MWENGE WA UHURU 2025

...
Mkuu wa Mkoa wa Lindi Zainab Telack akikagua Jengo la kituo cha Polisi Nandagala Mkoani Lindi

Na Regina Ndumbaro- Lindi

Mkoa wa Lindi uko tayari kuupokea Mwenge wa Uhuru mwaka 2025, ambapo maandalizi mbalimbali yamekamilika ikiwa ni pamoja na ukaguzi wa miradi itakayopitiwa na mbio hizo muhimu za kitaifa. 

Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mhe. Zainab Telack, ametembelea na kukagua miradi inayotarajiwa kupitiwa na Mwenge huo wilayani Ruangwa, ambapo ameonesha kuridhishwa na maendeleo na utekelezaji wake.

Katika ukaguzi huo, Mhe. Telack ametembelea mradi wa ujenzi wa barabara ya Mwilahi katika Kijiji cha Likangara yenye urefu wa mita 650, mradi unaogharimu zaidi ya Shilingi Milioni 513. 

Aidha, amekagua mradi wa dampo salama unaotekelezwa na kikundi cha vijana wa usafi wa mazingira katika Kijiji cha Lipande wenye thamani ya Shilingi Milioni 15. 

Mradi mwingine ni ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa na ofisi moja katika Shule ya Msingi Dodoma, Kata ya Nachingwea, wenye thamani ya Shilingi Milioni 48.

Miradi mingine mikubwa inayotarajiwa kupitiwa na Mwenge wa Uhuru ni pamoja na mradi wa maji katika Kijiji cha Mpara, Kata ya Likunja, unaojumuisha uchimbaji wa visima na ujenzi wa miundombinu ya maji kwa gharama ya zaidi ya Shilingi Milioni 325. 

Vilevile, Mwenge utatembelea ujenzi wa Kituo cha Polisi Nandagala chenye thamani ya Shilingi Milioni 164 na Kituo cha Afya Namakuku, ambapo Mwenge utaweka jiwe la msingi kwenye jengo la OPD lenye thamani ya zaidi ya Shilingi Milioni 153.

Aidha, Mwenge wa Uhuru pia utaweka jiwe la msingi kwenye mradi mkubwa wa ujenzi wa Shule ya Sekondari Namakuku, mradi unaogharimu zaidi ya Shilingi Milioni 591.

 Hii ni ishara ya dhamira ya Mkoa wa Lindi ya kuboresha huduma za kijamii kama elimu, afya, usalama na mazingira kwa manufaa ya wananchi wake.

Kwa mujibu wa ratiba rasmi, Mwenge wa Uhuru unatarajiwa kupokelewa Mei 28, 2025 katika Kijiji cha Namichiga, ambapo utapitia miradi yote iliyotajwa na hatimaye kukesha katika Kijiji cha Nandagala wilayani Ruangwa. 

Mkoa wa Lindi unaendelea kujiandaa kikamilifu kuhakikisha tukio hilo linafanyika kwa mafanikio makubwa.  


Jengo la Kituo cha Polisi Nandagala ambacho ni miongoni mwa miradi iliyokaguliwa na Mkuu wa Mkoa wa Lindi Mhe. Zainab Telack
Mkuu wa Mkoa wa Lindi Zainab Telack akiwa na baadhi ya viongozi Mkoani Lindi wakati wa Ukaguzi wa miradi mbalimbali na maandalizi ya kuupokea Mwenge tarehe 28 March Mwaka huu
Mkuu wa Mkoa wa Lindi Zainab Telack akiwa anatembea kwaajili ya kukagua miradi kwa ukaribisho na maandalizi ya Mwenge wa uhuru Mkoani Lindi
Share:

Related Posts:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © 2025 MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger