Na Woinde Shizza , Arusha
Tanzania imeorodheshwa katika kundi la juu la nchi 46 duniani zilizofanikiwa kuwa na viwango bora vya usalama mtandaoni, hatua inayochangia kuvutia idadi kubwa ya wawekezaji wanaotaka kuwekeza nchini.
Taarifa hiyo imetolewa na Taasisi ya Kimataifa ya Usalama Mtandaoni – Global Cybersecurity Index (GCI) kwa mwaka 2024, na imewasilishwa katika Jukwaa la Nne la Usalama Mtandaoni nchini Tanzania linalofanyika jijini Arusha.
Akizungumza katika jukwaa hilo, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT Commission), Dkt. Nkundwe Mwasaga, amesema mafanikio hayo yanatokana na juhudi za serikali ya awamu ya sita katika kujenga uchumi wa kidijitali na kuimarisha mifumo ya ulinzi wa kimtandao.
Aidha, Dkt. Mwasaga ameeleza kuwa serikali ipo katika hatua za mwisho za kukamilisha ujenzi wa kituo cha kuchakata masuala ya usalama mtandaoni (Digital Technology Institute) huko Dodoma, ambacho kitaongeza ufanisi katika kulinda miundombinu ya kidijitali.
Kwa upande wake, mdau wa usalama mtandao Robert Karamagi amesema kwa sasa kuna maendeleo makubwa ya matumizi ya mifumo ya kidijitali, ikiwemo teknolojia ya akili bandia (AI), katika sekta za afya, elimu, biashara na sheria.
Naye mtaalamu wa usalama mtandaoni na uchunguzi wa makosa ya kimtandao, Yusuph Kileo, amesema mkutano huo ni muhimu kwani umewakutanisha wataalamu wa usalama wa mtandao kutoka ngazi ya kitaifa na kimataifa kujadili changamoto mbalimbali na kutafuta suluhu ya pamoja.
“Binafsi, katika jukwaa hili nitawasilisha mada mahususi kuhusu intelijensia ya uhalifu wa kimtandao, ambapo tutaangazia sababu mbalimbali zinazochochea ongezeko la uhalifu huu, na kwa pamoja kujadili mbinu za kukabiliana na changamoto hizo ambazo zinaathiri si tu wizi wa data na fedha, bali pia maeneo muhimu ya jamii,” alieleza Kileo.
Aliongeza kuwa kwa mujibu wa utafiti wa kimataifa wa mwaka 2024, uhalifu wa kimtandao unagharimu dunia dola trilioni 10.5, kiasi ambacho ni hasara kubwa kwa uchumi wa dunia.
Jukwaa la Nne la Usalama Mtandaoni nchini Tanzania limewakutanisha wadau kutoka serikalini, sekta binafsi, taasisi za elimu, mashirika ya kiraia na washirika wa kimataifa.
0 comments:
Post a Comment