Wednesday, 9 April 2025

MAONESHO YA MADINI MKOA WA LINDI KUFANYIKA JUNI 11 HADI 14, 2025

...

Na Regina Ndumbaro-Lindi.

Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mhe. Zainab Telack, ameongoza kikao cha kwanza cha maandalizi ya Maonesho ya Madini yaliyopangwa kufanyika kuanzia Juni 11 hadi 14, 2025 katika viwanja vya madini vilivyopo Ruangwa, mkoani Lindi. 

Maonesho hayo ni msimu wa pili kufanyika katika mkoa huo na yataambatana na mnada mkubwa wa madini. 

Kikao hicho kimefanyika Ruangwa na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali, wawakilishi wa makampuni ya uchimbaji na uchenjuaji wa madini, wachimbaji wadogo, taasisi za Serikali na kifedha, pamoja na wadau wengine muhimu wa sekta ya madini.

Katika kikao hicho, Mhe. Telack amesema kuwa maonesho ya mwaka huu yatakuwa ya kipekee na tofauti na yale yaliyotangulia. 

Ametoa wito kwa kila mdau kushiriki kikamilifu kwa nafasi yake ili kufanikisha tukio hilo muhimu. 

Miongoni mwa waliokutana katika kikao hicho ni pamoja na wawakilishi wa Bodi ya Korosho, vyama vya ushirika kama Lindi Mwambao na RUNALI, ambao wote kwa pamoja wameonesha utayari wa kushiriki katika maandalizi na utekelezaji wa maonesho hayo.

Maonesho hayo yanatarajiwa kuwa jukwaa muhimu kwa ajili ya kutangaza fursa za madini zinazopatikana mkoani Lindi, kuimarisha usimamizi wa rasilimali hizo, na kuhamasisha uwekezaji endelevu. 

Lengo kuu ni kukuza uchumi wa wananchi wa Mkoa wa Lindi pamoja na Taifa kwa ujumla kwa kuhakikisha rasilimali za madini zinatumika kwa manufaa ya watu wote.

Mhe. Telack amesisitiza pia kuhusu umuhimu wa mnada mkubwa wa madini utakaoambatana na maonesho hayo, ambao utatoa nafasi kwa wachimbaji na wadau wa madini kuuza, kununua, na kuona vito mbalimbali vya thamani vinavyopatikana mkoani Lindi. 

Hii ni fursa muhimu kwa sekta ya madini kuonyesha thamani yake halisi na kuwavutia wawekezaji wapya ndani na nje ya nchi.

Share:

Related Posts:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © 2025 MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger