Na Mwandishi Wetu
Absa Bank Tanzania imezindua rasmi Akaunti ya Mzawa, huduma kamili ya kibenki kwa Watanzania waishio, wanaofanya kazi na kusoma nje ya nchi.
Uzinduzi huo umefanyika katika Hoteli ya Hyatt Regency jijini Dar es Salaam kwa njia ya mseto (“phygital”) ambapo wadau muhimu walihudhuria ana kwa ana huku wengine wengi kutoka ughaibuni wakijiunga kwa njia ya mtandao.
Akaunti ya Mzawa imelenga kuondoa changamoto zilizodumu kwa muda mrefu zinazowakabili Watanzania waishio nje ya nchi, ikiwa ni pamoja na ugumu wa kupata huduma za kifedha, changamoto za kufungua akaunti za fedha za kigeni, pamoja na upungufu wa taarifa za fursa na msaada wa mbali. Huduma hii inatoa upatikanaji wa kimataifa wa akaunti kwa sarafu tano (TZS, USD, GBP, EUR, na ZAR), kufanikisha miamala rahisi, fursa za uwekezaji, na huduma za bima kupitia Absa Bima.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Mgeni rasmi katika hafla hiyo Naibu Waziri wa Mambo ya Nje Cosato David Chumi alikiri mchango mkubwa wa diaspora pamoja na changamoto wanazokumbana nazo: “Diaspora yetu haijajitenga – imewekeza kwa dhati.
Lakini kwa bahati mbaya, hawapati fursa za kutosha kushiriki ipasavyo. Na sisi kama serikali tunasema tumewasikia. tunawaona. na tunachukua hatua. Chini ya uongozi wa . Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, serikali imepiga hatua kubwa kupitia huduma za ubalozi kwa njia ya kidijitali, majukwaa ya uwekezaji ughaibuni, na sasa kuhimiza mabenki kama Absa kuunda huduma mahsusi kwa diaspora.”
Naibu Waziri pia alipongeza Absa kwa kutoa suluhisho la wakati, jumuishi na lenye tija: “Akaunti ya Mzawa ya Absa inaleta pamoja kila kitu ambacho diaspora imekuwa ikikiomba. Kwa Watanzania wote waishio nje ya nchi, nawaambia: muda ni huu. Miundombinu inajengwa. Msaada unazidi kuongezeka. Tuchukue hatua sasa – tujenge nyumba, tufungue biashara, tuwekeze, na tujikite nyumbani Tanzania.”
Uzinduzi wa Akaunti ya Mzawa unaendeleza pia huduma ya awali ya Mkopo wa Nyumba kwa Diaspora kutoka Absa, ikiwapa Watanzania wa ughaibuni uwezo wa kudhibiti fedha zao huku wakiwekeza kwenye maendeleo ya muda mrefu nyumbani.
Kwa kuzingatia ahadi yake ya chapa, “Stori yako ina thamani’” na dhamira ya shirika “Kuiwezesha Afrika ya Kesho, pamoja, stori moja baada ya nyingine”, Absa Bank Tanzania inaendelea kutoa suluhisho bora zinazomlenga mteja, ili kuwaunganisha Watanzania wote na fursa zilizopo nyumbani – popote walipo duniani.
Kwa mujibu wa takwimu kutoka Idara ya Masuala ya Diaspora, inakadiriwa kuwa zaidi ya Watanzania 400,000 wanaishi nje ya nchi, wakiwa wengi wao wako Marekani, Uingereza, Kanada, Ulaya, Mashariki ya Kati, na kusini mwa Afrika. Mwaka 2022 pekee, Watanzania waishio ughaibuni walituma zaidi ya USD milioni 598 kurudi nyumbani, sawa na zaidi ya TSh trilioni 1.4, huku zaidi ya TSh bilioni 6.4 zikitumika kununua mali.
0 comments:
Post a Comment