Friday, 25 April 2025

SARATANI YA MLANGO WA KIZAZI BADO NI TISHIO LICHA YA JUHUDI ZA SERIKALI

...


Na Dotto Kwilasa, Dodoma

Licha ya jitihada zinazoendelea kufanywa na serikali kupitia Wizara ya Afya na wadau mbalimbali, saratani ya mlango wa kizazi bado imeendelea kuwa tishio kubwa kwa afya ya wanawake nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari Aprili 24, 2025 jijini Dodoma katika wiki ya chanjo kitaifa, Kaimu Meneja wa Mpango wa Taifa wa Chanjo, Lodalis Gadao, amesema saratani hiyo huanzia kwenye mlango wa kizazi – sehemu inayounganisha mfuko wa uzazi na uke – kutokana na seli kukua kwa kasi isiyo ya kawaida.

Takwimu kutoka Taasisi ya Saratani ya Ocean Road zinaonyesha kuwa takriban asilimia 36 ya vifo vinavyotokana na saratani nchini husababishwa na aina hii. Kila mwaka, zaidi ya wanawake 100,000 huambukizwa, huku zaidi ya 6,000 wakipoteza maisha.

Gadao ameeleza kuwa changamoto kubwa ni uelewa mdogo na mwitikio hafifu wa wanawake kujitokeza kwa uchunguzi na kupata chanjo ya HPV. Zaidi ya asilimia 70 ya wagonjwa hufika hospitalini wakiwa katika hatua za mwisho, hali inayopunguza mafanikio ya matibabu.

Ametaja wanawake wanaoishi na VVU na watoto wa kike wanaoanza ngono katika umri mdogo kuwa katika hatari kubwa zaidi ya kupata ugonjwa huo. Uchunguzi umebainisha kuwa kati ya wasichana wanne wanaojihusisha na mapenzi mapema, watatu huambukizwa.

Mikakati ya kudhibiti ugonjwa huo inahusisha utoaji wa chanjo kwa watoto wa kike kuanzia miaka 9 na kuelimisha jamii kuhusu madhara ya kuwa na wapenzi wengi.

Dk. Tumaini Haonga, Afisa wa Programu ya Elimu kwa Umma, alisema baadhi ya walengwa wanashindwa kupata chanjo kutokana na changamoto kama kuhama hama kwa wakulima na wafugaji, au wazazi wa mijini kukosa muda wa kuwapeleka watoto wao.

Wizara imehimiza jamii kushiriki kikamilifu katika kutoa elimu ya afya ya uzazi, na kuwasisitiza wanawake kufanyiwa uchunguzi mara kwa mara ili kugundua ugonjwa huo mapema na kupata tiba stahiki.








Share:

Related Posts:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © 2025 MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger