Friday 3 December 2021

WAHUNI 12 WANAOKWAPUA SIMU KWA BODABODA WAKAMATWA

...


Jeshi la Polisi katika Kaunti ya Kiambu nchini Kenya, imefanikiwa kukamata simu zaidi ya 30 na watuhumiwa 12 wa matukio ya uporaji wa simu, wengi wakiwa ni wale wanaotumia bodaboda na visu kufanya uhalifu huo.

Watuhumiwa hao wamekamatwa katika oparesheni maalum iliyoendeshwa na Jeshi la Polisi nchini Kenya katika maeneo ya Githogoro, Murera na Kiambu ambapo watuhumiwa hao, hujifanya ni madereva bodaboda kabla ya kuwapora abiria na watembea kwa miguu simu zao.

Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi Kaunti ya Kiambu, Mohamed Badel amesema watuhumiwa hao, hufurika katika mitaa ya Mji wa Kiambu kuanzia majira ya saa kumi alfajiri hadi saa kumi na moja, muda ambao watu wengi hutoka majumbani mwao kuelekea makazini.

Badel amesema waliamua kuendesha oparesheni maalum baada ya kusikia malalamiko ya mara kwa mara ya wakazi wa mji huo ambapo kwa kushirikiana na wasamaria wema, walifanikiwa kuwanasa wahalifu hao.

Ameongeza kuwa watuhumiwa wote wapo rumande na wanatarajiwa kufikishwa katika Mahakama ya Kiambu kusomewa mashtaka yanayowakabili na kuwataka madereva wa bodaboda wanaozingatia sheria, kujiandikisha na kupewa namba maalum zitakazowatofautisha na wahalifu.

Pia amewataka watu walioibiwa simu zao, kufika katika Kituo cha Polisi cha Kiambu ili kuzitambua simu zao.
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger