Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Watu wenye Ulemavu), Mhe.Ummy Nderiananga akizungumza na watumishi wa Shirika la Bima la Taifa (NIC) wakati akifungua mpango wa mafunzo ya usalama na afya kwa watumishi wa umma ulioanza kutekelezwa na OSHA kwa NIC ambapo utaendelea kutekelezwa kwa Taasisi nyingine za Serikali na Mashirika ya Umma.
Mkurugenzi wa Usalama na Afya wa OSHA, Alexander Ngata akiwasilisha taarifa fupi ya mpango wa mafunzo ya usalama na afya kwa watumishi wa umma unaotekelezwa na OSHA wakati wa ufunguzi wa mpango huo uliozinduliwa na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Watu wenye Ulemavu) Mhe. Ummy Nderiananga (Katikati). Wakwanza kulia ni Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa Shirika la Bima la Taifa, Lihami Masoli.Mkaguzi wa afya wa OSHA, Dkt. Amin Vasomana akimpima afya mtumishi wa Shirika la Bima la Taifa (NIC) wakati wa ufunguzi wa mpango wa mafunzo ya usalama na afya kwa watumishi wa umma uliombatana na zoezi la upimaji afya kwa washiriki wa mafunzo hayo.
Mkufunzi wa mafunzo ya huduma ya kwanza wa OSHA, Hans Mpera, akionesha namna ya kumpa huduma ya kwanza mtu aliyejeruhiwa kichwani, wakati wa mafunzo ya usalama na afya kwa watumishi wa Shirika la Bima la Taifa (NIC) yanayofanyika Mkoani Morogoro.
******************
Na Mwandishi Wetu
Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) umezindua rasmi mpango wa mafunzo ya Usalama na Afya kwa Taasisi za Serikali na Mashirika ya Umma Tanzania Bara.
Mpango huo ambao umeanza kutekelezwa kwa kutoa mafunzo kwa watumishi wa Shirika la Bima la Taifa (NIC) umezinduliwa na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Watu wenye Ulemavu), Ummy Nderiananga ambaye amezitaka Taasisi nyingine za serikali kujiandaa kutekeleza mpango huo.
“Natoa pongezi za dhati kwa menejimenti ya NIC kwakutambua umuhimu wa mafunzo haya na kuamua kushirikiana na Taasisi yetu ya OSHA katika kufanikisha jambo hili muhimu. Hivyo basi, niwasihi nyote mnaoshiriki mafunzo haya kuyazingatia na kwenda kuyatumia ipasavyo katika kuboresha utendaji wenu wa kila siku,” alisema Mhe. Naibu Waziri na kuongeza:
“Aidha, niwaagize OSHA kuhakikisha kwamba wanayafikia Mashirika na Taasisi zote za serikali na kutoa mafunzo ya Usalama na Afya kwa watumishi wote ambapo ni matumaini yetu kwamba endapo yatatolewa na kutekelezwa kikamilifu basi yatasaidia kupunguza ajali, magonjwa na vifo vitokanavyo na mazingira ya kazi yasiyo rafiki. Hii itaisaidia serikali kuepuka gharama za kuwahudumia majeruhi wa ajali na wagonjwa pamoja na kuepuka hasara kubwa ambayo Taifa limekuwa likipata kutokana na kupoteza nguvukazi yake pamoja na uharibifu wa mali na miundombinu mbalimbali za uzalishaji.”
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa mpango huo, Mkurugenzi wa Usalama na Afya wa OSHA, Alexander Ngata, ametoa wito kwa Taasisi mbalimbali za serikali kushirikiana na OSHA ili kufanikisha utekelezaji wa mpango huo ambao unahusisha ukaguzi wa usalama kwenye maeneo ya kazi pamoja na uchunguzi wa afya za wafanyakazi.
“Nitoe wito kwa waajiri katika sekta ya umma kutenga bajeti kwa ajili ya kutoa mafunzo ya usalama na afya kwa watumishi wao zoezi ambalo tutaliendesha sambamba na ukaguzi wa mifumo ya usalama na afya kwenye maeneo yao ya kazi pamoja na kuchunguza afya za wafanyakazi kama tulivyofanya kwa Shirika la Bima la Taifa (NIC),” alisema, Bw. Ngata.
Kwa upande wa washiriki wa mafunzo hayo ambao ni viongozi wa NIC wameipongeza OSHA kwa kuja na mpango huo ambao wameuelezea kuwa ni mpango mzuri ambao mbali na kulinda afya na usalama wa wafanyakazi utaleta tija katika biashara na uzalishaji.
“Niwapongeze OSHA kwa kazi nzuri wanayofanya na niwaombe wajitahidi kuwafikia waajiri wengi zaidi kwani wakifanya hivyo hali ya usalama na afya itazidi kuimarika nchini jambo ambalo litatusaidia kuimarisha mifuko ya bima kutokana na kupungua kwa gharama za fidia za majanga mbalimbali,” alieleza Bw. Lihami Masoli, Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa NIC ambaye alishiriki mafunzo ya Huduma ya Kwanza yaliyotolewa na OSHA kwa menejimenti ya shirika pamoja na watumishi wengine.
Mshiriki mwingine wa mafunzo hayo, Bi. Florence Samweli, amesema mafunzo hayo ni mazuri na ni muhimu sana hususan kwa wafanyakazi katika maeneo mbalimbali ya kazi.
“Kwakweli mafunzo haya yakitolewa kwa watu wengi yatasaidia sana kuokoa maisha ya watu pindi ajali zinapotokea. Binafsi yamenijenga sana na naweza kusema baada ya kuhitimisha mafunzo haya sipo kama nilivyokuja hapo awali,” amesema Bi. Florence.
Miongoni mwa majukumu ya OSHA ni pamoja na kukuza uelewa wa masuala ya Usalama na Afya miongoni wa Watanzania kupitia kutoa mafunzo mbalimbali ikiwemo mafunzo ya Huduma ya Kwanza mahali pa kazi, Mafunzo kwa wanakamati za Usalama na Afya mahali pa kazi, Uchunguzi wa Ajali mahali pa kazi, Tathmini ya Vihatarisha vya Usalama na Afya mahali pa kazi pamoja na kozi nyinginezo zinazohusu masuala ya usalama na afya mahali pa kazi.
0 comments:
Post a Comment