Thursday, 30 December 2021

NAIBU WAZIRI ATOA SIKU 14 KWA KIWANDA KUREKEBISHA MFUMO WA MAJI TAKA

...

Kiwanda cha Hengji Investment Ltd cha Jijiji Dar es Salaam hii leo Desemba 30, 2021 kimepewa siku 14 kuhakikisha kinaweka mfumo wa kutibu maji taka kabla ya kuyatiririsha kwenye mazingira kufuatia agizo lililotolewa na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Hamad Chande (hayupo pichani)

Bomba la maji taka kutoka Kiwanda cha Hengji Investment Ltd cha Jijini Dar es Salaam, likitiririsha maji taka kwenye mto Ng’ombe kabla ya kuyatibu. Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Hamad Chande (hayupo pichani) ametoa siku 14 kwa kiwanda hicho kurekebisha dosari hiyo.

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Hamad Chande akizungumza na Askofu Allen Sisso wa Kanisa la Methodist Tanzania katika eneo la Boko, Dar es Salaam. Naibu Waziri Chande leo Desemba 30, 2021 amefanya ziara ya kukagua mwendelezo wa usafishaji mto huo kwa kuondoa mchanga, tope na taka ngumu katika eneo la Boko na kuagiza kasi iongezwe na kuandaa mpango wa muda mrefu ikiwa ni pamoja na ujenzi wa kingo za mto ili kukabiliana na mafuriko katika eneo hilo.

******************************

Na Lulu Mussa -Dar es Salaam

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Hamad Chande leo Desemba 30, 2021 amefanya ziara ya kushtukiza katika Kiwanda cha kurejeleza mifuko cha Hengji Investment Co. Ltd kilichopo eneo la Ubungo, Dar es Salaam na kushuhudia ukiukwaji mkubwa wa Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004 kwa wamiliki wa kiwanda hicho kutiririsha maji taka ambayo hayatibiwa na bila kibali cha Mamlaka ya Bonde la Wami Ruvu kwenye Mto ng'ombe

Kufuatia ukiukwaji huo wa Sheria Naibu Waziri Chande ametoa siku 14 kwa Kiwanda hicho kuhakikisha kinaweka mfumo sahihi wa kutibu maji taka kabla ya kuyatiririsha kwenye mazingira kama Sheria inavyoelekeza na kupata kibali kutoka Mamlaka ya Bonde la Wami Ruvu.

"Wataalamu wa NEMC simamieni hili kikamilifu, nitarudi tena kukagua. Hatuwezi kuweka maisha ya wananchi rehani kwa kuruhusu ukiukwaji wa Sheria" Alisisitiza Naibu Waziri Chande.

Pia, amemuagiza Meneja wa Kiwanda cha Hengji Investment Bw. Calvin Payovela kuhakikisha wafanyakazi wa kiwanda hicho wanapatiwa vifaa vya usalama mahala pa kazi na kusisitiza kuwa hilo ni takwa la kisheria na si maamuzi ya mtu binafsi.

“Wafanyakazi hawa wapewe vifaa vya kujikinga na vumbi na afya zao kwa ujumla maana afya zao ni jambo muhimu sana, ili tuwe na kizazi endelevu yatupasa kuwa vijana wenye nguvu kazi ya kutosha” Alisisitiza Naibu Waziri Chande.

Meneja wa Kiwanda hicho Bw. Calvin Payovela amesema kuwa watahakikisha wanatekeleza maelekezo ya Serikali ndani ya muda uliotolewa.

Katika hatua nyingine Naibu Waziri Mhe. Hamad Chande ameuagiza uongozi wa Bonde la Wami Ruvu na Manispaa ya Kinondoni kuandaa mpango wa muda mrefu wa kunyosha Mto Nyakasanga ili kupunguza athari za mafuriko kwa wakazi wa eneo hilo. Naibu Waziri Chande ametoa rai hiyo baada ya kufanya ziara ya kukagua mwendelezo wa usafishaji mto huo kwa kuondoa mchanga, tope na taka ngumu katika eneo la Boko. Amesema Mamlaka ya Bonde la Wami Ruvu wana wajibu wa kuendelea kusimamia Sheria na kuhakikisha wananchi hawaweki makazi ya kudumu pembezoni mwa mto huo na kutoa elimu kwa umma juu ya namna bora ya kujikinga na athari zinazoweza kutokea kutokana na mto kupanuka.

"Lengo la Serikali ni kuhakiksha watu wako salama na mto unabaki salama" Chande alisisitiza. Kwa upande wake Kaimu Meneja wa Kanda ya Mashariki Kaskazini Bi. Lilian Kapakala amesema jamii inapaswa kupanda miti rafiki kwa mazingira pembezoni mwa mito ili kupunguza kasi ya mmomonyoko wa udongo.

Nae Mhaidrolojia kutoka Mamlaka ya Bonde la Wami Ruvu Bw. Jeremia Nestory amesema Mamlaka ya Bonde kwa kushirikiana na Manispaa ya Kinondoni wanaendelea na utekelezaji wa kusafisha Mto Nyakasanga kwa kuondoa tope na mchanga ili kurejesha mto katika mkondo wake.

Kufuatia uchimbaji holela wa mchanga kwenye mito na mabonde katika Mkoa wa Dar es Salaam umeandaliwa mwongozo wa usafishaji mchanga, tope na taka ngumu kwenye mito na mabonde kwa jiji la Dar es Salaam ambao utekelezaji wake umeanza.

Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger