Taarifa zilizotufikia hivi punde zinasema mwanamuziki mahiri wa Rhumba Le General Defao Matumona amefariki dunia akiwa nchini Cameroon Taarifa zaidi tutawaletea hivi punde
Defao alizaliwa Desemba 03, 1958 katika jiji la Kinshasa huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Baada ya kuzaliwa akapewa majina ya Mutomona Defao Lulendo.
Ni mwanamuziki mwenye talanta za kutunga na kuimba kwa sauti nyembamba na nyororo. Defao alianza kujishughulisha na muziki mwaka 1976, akiwa katika bendi ya Orchestra Suka Movema. Baadaye akaenda kujiunga katika bendi ya Fogo Stars.
Mwaka 1978 Defao akaenda kupiga muziki katika bendi ya Korotoro huko Somo, Magharibi mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC).
Alikuwa mmoja kati ya wanamuziki waliounda bendi mpya ya Grand Zaiko Wawa mwaka 1981, ikiongozwa na mpiga gitaa mashuhuri Pepe Felix Manuaku.
Katika kile kilichoitwa mbinu za kujitafutia maisha, Defao aliungana na mwanamuziki Ben Nyamabo kuunda kikosi kipya cha Choc Stars.
Bendi hiyo ya Choc Stars na Orchestra Shakara Gagna Gagna, zilikuwa chini ya uongozi wa Jeanpy Wable Gypson, zilimfanya General Defao kuwa maarufu kwa mara kwanza kitaifa.
Akiwa na wanamuziki akina Ben Nyamabo, Debaba, Carlito, Bozi Boziana na Djuna Djunana, bendi ya Choc Stars ikajizolea umaarufu mkubwa kupitia tungo zao.Uimbaji na uwajibikaji jukwaani wa General Defao aliweza kuonesha kuwa kipaji chake siyo cha kubahatisha.
Defao Mutomona kwa kawaida alicheza sambamba na wanenguaji wake, ambapo huwa kivutio kikubwa cha wapenzi na mashabiki wake akicheza mitindo mbalimbali ukiwemo ule wa ‘Ndombolo’ pasipo kuchoka.
Mutomona ilipofika mwishoni mwa mwaka 1990, aliiacha bendi hiyo ya Choc Stars, akiwa na madhumuni ya kuunda bendi yake.Dhamira yake alitimia baada ya kuunda bendi yake iliyopewa jina la Big Stars.
Katika bendi hiyo alipiga muziki kwa kushirikiana na mwimbaji mwingine Djo Poster, aliyetokea katika bendi ya Grand Zaiko.
Defao aliomuongeza katika safu ya wanamuziki mpiga solo chipukizi Jagger Bokoko, ambaye alitokea kuwa kipenzi chake kikubwa.
Bendi ya Big Stars ilikuwa na wanamuziki wengi wenye uwezo mkubwa wa kutengeneza muziki.
Kulikuwa na waimbaji akina Djo Djo Bayenge, Debleu Kinanga na Adoli Bamweniko.Kwa upande wa wapiga magitaa, kulikuwa na Mogus aliyekuwa akilicharaza gitaa la solo, gita la besi likiungurumishwa na Guy wa Nzambi.
Tumba zilikuwa zikidundwa na Richa Cogna Cogna. Mbofya kinanda alikuwa ni Sedjo Kavanda.
Katika kipindi cha miaka mitano ya bendi ya Big Stars, Defao alionesha ubunifu uliomletea mafanikio makubwa baada ya kufyatua album zisizopungua 17. Kati ya hizo, sita ziliingia katika soko la Ulaya mwaka 1995.
Mifarakano katika sehemu za kazi huwa hazikosi. Big Stars iliteteleka kwa kipindi kifupi mara baada ya kuondoka Djo Djo Bayenge na kumuacha Defao akiwa kiongozi wa bendi hiyo.
Defao akiwa na wanamuziki wake wa Big Stars, walikarabati upya bendi yao na kuweza kutengeneza kikosi kipya chenye wanamuziki mahiri. Walimuongeza Roxy Tshimpaka.
Roxy kabla ya kujiunga na Big Stras alikuwa katika bendi ya Choc Stars.
Aidha alimpata mwimbaji mpya Azanga.Siku zilivyokuwa zikiiendela, mpigaji gitaa la solo Jagger Bokoko akawa kuwa kipenzi kikubwa cha Defao.
Umaarufu wa General Defao ulizagaa maeneo mengi Afrika Mashariki na Kati kwenye miaka 1990.
Wapenzi na mashabiki wake waliulinganisha umaarufu wake na ule wa wanamuziki akina Papa Wemba, Koffi Olomide, Bozi Boziana na Kester Emeneya.
Hapana ubishi kwamba Defao Mutomona ni mwanamuziki aliye na umaarufu mkubwa miongoni mwa wanamuziki toka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Mpenzi msomaji utakubaliana nami iwapo utasikiliza nyimbo za Georgina, Fammilie Kikuta, Nadine, Bana Kongo, Oniva na Filie.
Nyimbo hizo ziko katika kiwango cha juu na zimepigwa katika mitindo miwili ya rumba na sebene mold.
Kufuatia uangalizi wa uzalishaji wa kazi toka kwa meneja wake kuwa mbovu, Defao alilazimika kubadili maprodyuza na kampuni za kurekodia.
Wakati mwingine alikuwa akitoka na matoleo ya kazi zake zilezile kwa lebo tofauti.
Defao alilivunja kundi zima la Big Stars mwaka 2000 wakiwa katika jiji la Kinshasa.
Yeye akaamua kwenda ‘kutanua’ katika jiji la Paris nchini Ufaransa wakati wa kipindi cha joto.
Lakini akiwa katika jiji hilo, alirekodi album ya Nessy de London, akiwashirikisha wanamuziki nyota waishio katika jiji hilo la Paris.
Wanamuziki hao walikuwa akina Nyboma Mwandido, Luciana de Mingongo, Wuta Mayi, Ballou Canta na Deesse Mukangi, walioshirikiana na Defao kufanya onesho kubwa lililo wavutia watu wengi.
Defao kwa kuwatumia waimbaji hao waalikwa, walipelekea album yake ya De London kupanda chati zaidi.
Aliachia album nyingine nyingi zikiwa na nyimbo za Mandova, Ya Gege, Copinnage, Sam Samita, Salanoki Guerre De1, Animation na Nessy of London.
Katika hali isiyokuwa ya kawaida, Defao baadae akawa kimya katika anga ya muziki.
Hali hiyo yasemekana kuwa ilitokana na sintofahamu ya kisiasa nchini mwake iliyopelekea kufungiwa kupiga muziki huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wakati wa uongozi wa Rais Lauler Kabila.
Defao alifika nchi za Afrika ya Mashariki ikiwemo Tanzania.
Katika ziara yake ya nchini Tanzania iligubikwa na matatizo lukuki mwaka 2000, uliokuwa mwaka mpya wa Millenium.Baada ya kumaliza kufanya maonyesho kadhaa, Defao alizidiwa akili na ‘Mapromota’ waliomleta, matokeo yake alifikia hadi kukosa pesa ya kujikimu pamoja na kulipia Visa yake kuwa mushkeri.
Nguli huyo ‘alifulia’ hata nauli ya kumrejesha kwao Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo hakuwa nayo.
Bahati njema ilikuwa upande wake kwa kuwa alifanikiwa kurejea kwao baada ya kupewa ‘lift’ katika ndege ya Shirika la Ndege la Tanzania (ATC), aliyokuwa ikizindua safari zake kati ya Dar es Salaam na Lubumbashi nchini DRC.
“Kimya kingi kina mshindo mkuu” usemi huu ulijionesha wazi kwa gwiji hilo lililosubiriwa na wapenzi kwa kipindi kirefu hadi mwaka 2006, ndipo alipotoka na album yake mpya yenye Lebo ya Nzombo le Soi.
Baada ya miaka minne mingine alifyatua CD yake yenye Lebo ya Pur Encore mwaka 2010.Mwaka 2012 Defao kwa bahati nzuri alirudi ulingoni akiwa na album ya The Undertaker.
0 comments:
Post a Comment