Friday 3 December 2021

GGML YATOA MILIONI 84 MAPAMBANO DHIDI YA VVU NA UKIMWI

...

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa (kulia) akimkabidhi cheti na ngao Makamu wa Rais wa Kampuni ya GGML anayeshughulikia miradi endelevu, Simon Shayo (kushoto) kwa kutambua mchango wa kampuni hiyo katika mapambano dhidi ya VVU na Ukimwi. Wanaoshuhudia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu ( Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye ulemavu) Jenista Mhagama (katikati) na Mkurugenzi wa TACAIDS, Dk. Leonard Maboko. GGML imekabidhiwa cheti hicho jana jijini Mbeya katika maadhimisho ya siku ya Ukimwi duniani yaliyofanyika kitaifa mkoani humo.

KAMPUNI ya Geita Gold Mining Limited (GGML) imechangia zaidi ya Sh milioni 84 kusaidia mipango ya serikali katika mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya UKIMWI Duniani yaliyofanyika kitaifa jijini Mbeya. 


GGML na Tume ya Kudhibiti Ukimwi (TACAIDS), kupitia Kampeni ya Kilimanjaro Challenge, wanashirikiana kwa namna mbalimbali ikiwamo kuongeza uelewa kuhusu janga la VVU na UKIMWI ili siku moja Tanzania itangazwe kuwa imetokomeza kabisa janga hilo katika ukanda huu wa Afrika Mashariki.


Akizungumza katika Maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani juzi jijini Mbeya, Makamu wa Rais wa GGML anayeshughulikia miradi endelevu, Simon Shayo alisema kaulimbiu ya mwaka huu isemayo “Zingatia Usawa, Tokomeza Ukimwi, Tokomeza magonjwa ya mlipuko,” ni muhimu kwa jamii ya Geita na Tanzania kwa ujumla.


Alisema mpango wa GGML Kili Challenge ni mradi mahsusi kutoka katika sekta binafsi ambao umeisaidia serikali kwa zaidi ya miaka 20 katika mapambano dhidi ya VVU.


“Kupitia mpango huu, wachangiaji wenzetu wameendelea kuwa mstari wa mbele kudhibiti janga la VVU kwa kuhakikisha utoaji huduma za kimatibabu unazingatia utu na haki za wale wote wanaoweka imani yao kwetu hususani wale walio hatarini zaidi.


“Tunaziomba sekta binafsi nchini kuungana na GGML na kusaidia mfuko wa Ukimwi ili kuwezesha mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI kuwa endelevu. Bila kuwa na mipango imara ya kuhakikisha usawa katika utoaji wa huduma hizi za kimatibabu ni dhahiri duniani itashindwa kufikia lengo lake la kutokomeza Ukimwi ifikapo mwaka 2030”, alisema.

Kama raia anayewajibika, GGML pia iliandaa kampeni ya upimaji wa VVU kwa hiari kwa wiki mbili ikilenga kufikia asilimia 80 ya wafanyakazi wake 5000. Hao ni wafanyakazi walioajiriwa moja kwa moja na wakandarasi.

Shayo aliongeza kuwa maendeleo chanya ya kijamii na kiuchumi ya mkoa na nchi yetu ni matokeo ya jamii yenye afya.


"GGML ni kampuni inayothamini mali na watu wake. GGML inaamini kuwa uwekezaji unaofaa katika afya ya wafanyakazi utaleta nguvu kazi yenye afya na kuongeza tija katika utendaji na ukuajiji wa kibiashara,” alisema Shayo.


Alisema kuanzia tarehe 1 – 14 Desemba 2021, GGML imealika jumla ya washauri nasaha 15 waliopata mafunzo ya UKIMWI kutoka serikalini na hospitali binafsi kufanya Upimaji wa VVU kwa hiari katika eneo lote la Mgodi.


“Ikiwa na wafanyakazi walioajiriwa na wakandarasi zaidi ya 5,000, GGML inawakilisha sehemu kubwa ya jamii ya Mji wa Geita ambao kama wakiwa wameelimishwa vya kutosha kuhusu VVU na UKIMWI, watakuwa na ushawishi chanya miongoni mwa jamii nzima ya Geita.

GGML Kilimanjaro Challenge dhidi ya VVU & UKIMWI ilizinduliwa zaidi ya miaka 20 iliyopita kwa lengo la kuongeza uelewa wa janga hili na kutoa msaada wa kifedha kwa mipango ya VVU na UKIMWI.

Tangu kampeni ya GGML Kilimanjaro Challenge ilizinduliwe miaka 20 iliyopita, zaidi ya watu 800 kutoka sehemu mbalimbali dunia wameshiriki kwa kupanda Mlima Kilimanjaro kwa njia ya kawaida na kuuzunguka mlima kwa kutumia baiskeli.

Kilimanjaro Challenge imebadilika na kushirikisha makampuni ya ndani na nje ya nchi na watu binafsi kutoka duniani kote hali iliyosaidia kuchangisha zaidi ya Sh bilioni 1.3 tangu 2018 kwa ajili ya miradi ya kinga, matunzo na matibabu ya VVU nchini kote.



Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger