Wednesday 27 May 2020

TAKUKURU Yaanza Kuichunguza CHADEMA Juu Ya Tuhuma Za Matumizi Mabaya Ya Fedha.

...
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (Takukuru), imeanza kuchunguza tuhuma za matumizi mabaya ya fedha, inazokikabili Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
 
Hivi karibuni, kumekuwepo na madai yanayotolewa na baadhi ya wabunge juu ya matumizi mabaya ya fedha walizochanga kila mwezi kwa mujibu wa Katiba.

Baadhi ya waliotoa shutuma hizo ni; wabunge wa viti maalum; Susan Maselle, Joyce Sokombi na Peter Lijualikali wa Kilombero ambao wote wametangaza kukihama chama hicho.

Kwa nyakati tofauti, wabunge hao, Maselle na Sokombi walisema mara baada ya Bunge kuvunjwa watahamia NCCR-Mageuzi huku wakisema, hawana shida na kuchangia fedha hizo lakini matumizi yake hayaeleweki.

Leo Jumatano, tarehe 27 Mei 2020, Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru  Brigedia Jenerali John Mbungo amesema wameanza kuwahoji baadhi ya watu.

 “Kwa mujibu wa taarifa tulizo nazo, kuna matumizi mabaya ya fedha za michango ya wanachama, ambayo kwa mujibu wa katiba yao wanadai imeanishwa wachangie.”

“Lakini, matumizi yake ndio wanatilia mashaka, kuna fedha nyingi zinatumika ndivyo sivyo, kwa mujibu wa makubaliano yao,” amesema Jenerali Mbungo.

“Kwa hiyo, tunachunguza matumizi yasiyo sahihi ya fedha zao, Takukuru inayomamlaka ya kuchunguza taasisi yoyote iwe ya umma, watu binafsi, chama, klabu, iwe chochote Takukuru wanaingia kufanya uchunguzi, ilimradi kuwe na ubadhirifu au matumizi mabaya ya fedha na rushwa,” amesema bosi huyo wa Takukuru.

Amesema, wameanza kuwahoji wanachama waandamizi  na viongozi wa Chadema, wabunge waliotoa tuhuma hizo, pamoja na maafisa wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Mbungo amewataja baadhi ya watakaohojiwa ni; Dk. Vincent Mashinji, aliyekuwa Katibu Mkuu Chadema, ambaye kwa sasa amehamia Chama cha Mapinduzi (CCM), John Mrema, Mkurugenzi wa Itifaki na Mambo ya Nje Chadema, pamoja na mhasibu mkuu wa chama hicho, Dk. Roderick Lutembeka.

Aidha, Jenerali Mbungo amesema wameshindwa kumhoji Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema Taifa, kuhusu sakata hilo, kwa kuwa aliieleza TAKUKURU kwamba yuko nje ya jiji la Dar es Salaam.

Amesema, taasisi hiyo imeshaanza kukusanya nyaraka mbalimbali, zinazohusiana na tuhuma hizo.

Credit: Mwanahalisi


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger