Tuesday 26 May 2020

Maafisa wawili wa TRA Manyara wadakwa na TAKUKURU kwa kumuomba Mteja wao Rushwa ya Milioni kumi

...
Na John Walter-Manyara
Mkuu  wa Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa mkoa wa Manyara (TAKUKURU) Holle Mkungu, amesema wanatarajia kuwafikisha katika Mahakama ya hakimu mkazi Manyara, maafisa wawili wa TRA mkoani hapa kwa makosa ya kudai na kupokea Rushwa ya shilingi Milioni kumi.

Amewataja watuhumiwa hao kuwa ni Subilaga Mwangama na Ojungu Mollel,  na kwamba  makosa hayo ni kinyume cha kifungu cha 15 cha sheria ya kuzuia na kupambana na Rushwa namba 11/2007.

 Akizungumza na  waandishi wa habari  ofisini kwake,  amesema kuwa Uchunguzi wa Takukuru  ulibaini kwamba mlalamikaji  (jina linahifadhiwa kwa sababu kwa za kiusalama)  ni mlipakodi mzuri kwa mamlaka ya mapato  kituo cha  wilaya ya Mbulu ambapo kwa kipindi  cha mwaka 2018 alilipa kodi zaidi ya million 9.

Hata hivyo mwezi machi 2020  mlalamikaji alipigiwa simu na washtakiwa  hao wakimtaka  afike ofisi za mamlaka ya mapato  mjini Babati,  ambapo mlalamikaji alifika na kukutana na  Maafisa  hao wawili kutoka mamlaka ya mapato Tanzania ambao walimfahamisha kuwa wamefanya ukaguzi wa biashara yake  na kugundua kuwa alikadiriwa  vibaya na hivyo kumtaka  kulipa ongezeko la zaidi ya shillingi millioni tano [Sh.5.812,544,00.]

Makungu ameeleza kuwa  mfanyabiashara huyo (mlalamikaji)  alikubali ongezeko hilo na alianza kulipa kwa awamu  baada ya kuomba na kukubaliwa kulipa kwa awamu na Meneja  wa mamlaka ya mapato Wilaya ya mbulu, ambapo uchunguzi wa Takukuru mkoani hapa ulibaini kuwa mlalamikaji akiwa amelipa awamu ya kwanza ya ongezeko hilo  na baadae alipigiwa tena simu na washitakiwa na kutakiwa kwenda Babati kwa ajili ya mahojiano kuhusu ulipaji kodi wa mwaka  huo  wa 2018 ambao ulikuwa tayari wamemkadiria ongezeko.

Aidha mlalamikaji huyo alikuwa na washitakiwa katika ofisi za mamlaka za mapato  Babati na akajulishwa kuwa kuna ongezeko tena kwenye kodi ya biashara yake ya kiasi cha shilingi millioni arobaini  na tano (45,000,000).

‘’Ongezeko hilo lilimuweka mfanyabiashara huyo  kwenye wakati mgumu  lakini hata hivyo washitakiwa walimpooza  mfanyabiashara huyo kwa maelezo  kuwa wanaweza kumpunguzia kutoka million 45  hadi kufikia ongezeko la million 9  endapo angekubali kutoa  rushwa’’alisema Makungu .

Hata hivyo uchunguzi wa Takukuru  uliendelea kubainisha kuwa mjadala wa kiasi gani  cha rushwa atoe ili apunguziwe ongezeko   uliendelea kati ya washtakiwa na mfanyabiashara  huyo, ambapo dau la shilingi  million 20 (20,000,000)  waliloanzia lilipungua hadi  kufikia million 10 (10,000,000)  ambapo mfanyabiashara huyo alielekezwa kuzipeleka  kwa mmoja wa mawakala waliopo mjini Babati  na ilipofikia hatua hiyo ndipo makachero wa Takukuru walipoandaa mtego uliopelekea watuhumiwa kukamatwa.

Hata hivyo mkuu wa TAKUKURU  mkoani hapa Holle Makungu   ametoa wito kwa mamlaka ya  ya mapato mkoa wa manyara  na Tanzania kwa ujumla  kwamba kuna haja ya kuangalia upya mfumo wa ulipaji  wa kodi ili kuwa na mfumo unaoeleweka kwa wafanyabiashara wote wa biashara za aina zote  ili kudhibiti vitendo vya rushwa na kuondoa mianya inayotumiwa  na baadhi ya maafisa wachache  wa mamlaka hiyo  waliokosa uadilifu kwa kuwabambikia wafanyabiashara kodi  zisizolipika  kwa nia ya kuwatisha  kisha kujipatia rushwa  kama walivyofanya watuhumiwa hao.


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger