Eric Msuya – MAELEZO
Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Kanali Wilbert Ibuge amewataka watanzania kuendelea kudumisha umoja na Ushirikiano wa Kibiashara katika ukanda wa Jumuiya ya maendeleo Kusini mwa Afrika SADC.
Akizungumza na waandishi wa Habari mara baada ya kufungua Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa SADC kwa ngazi ya Makatibu Wakuu uliofanyika kwa njia ya Mtandao (video conference) leo jijini Dar es Salaam, amesema Mkutano huo ni mahususi kwa kujadili na kuondoa vikwazo vyote vya Kibiashara ili kuweza kuendeleza Uchumi ndani ya Jumuiya.
“Kikao cha makatibu wakuu cha leo, kimekubaliana kuondoa kikwazo cha bidhaa mahususi tu kupita katika mipaka yetu badala yake bidhaa zote zinazowezesha wananchi wetu kuendelea na maisha ni lazima ziruhusiwe kupita katika mipaka ya nchi wanachama wa SADC” Amesema Balozi Ibuge
Aidha, Katibu Mkuu ameongeza kuwa ni muhimu wa wanaSADC kujumuika katika wakati huu na kuona ni jinsi gani wanaweza kushirkikiana na kuhakikisha kuwa Uchumi wa Nchi Wanachama wa SADC unakua na kuongeza juhudi za kibiashara kuendelea kufunguka.
“kwa mfano halisi sisi kama Tanzania hatukufunga mipaka yetu, na katika kutokufunga mipaka yetu bado tunatambua kwamba tunaendelea kuwategemea wenzetu kama wanavyotutegemea sisi, tuna bandari inayohudumia Nchi nane za SADC na zisizokuwa za SADC na ambazo ndizo hasa tunapozungumzia utengamano na mazingiara ya kufanya biashara na kuzingataia zile tahadhari mbalimbali ambazo nchi hizo zimekuwa zikichukua” amesema Balozi Ibuge
Mkutano huo wa siku tatu 27 hadi 29 Mei, 2019 unajadili Hali ya kifedha ndani ya Jumuiya, Utekelezaji wa Maazimio yaliyotokana na kikao cha Baraza la Mawaziri wa SADC ambayo ni Menejimenti ya Maafa, utekelezaji wa kaulimbiu ya Mkutano wa 39 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC isemayo "Mazingira Wezeshi kwa ajili ya Maendeleo Endelevu na Jumuishi ya Viwanda, Kukuza Biashara na Ajira ndani ya SADC" na mapitio ya hali halisi ya biashara baina ya nchi, maendeleo ya viwanda ndani ya Jumuiya na taarifa ya utekelezaji wa Mkakati wa Maendeleo ya Viwanda wa Jumuiya na Mpango kazi wake.
Pia, Mkutano huo unahusisha wataalamu kutoka nchi 12 wanachama wa SADC kutoka sekta za Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Fedha na Mipango, Uchukuzi na Mawasiliano, Viwanda na Biashara, Maliasili na Utalii pamoja na Afya. Mkutano huo pia utatoka na maazimio ambayo nchi wanachama watatakiwa kuyatekeleza ndani ya muda utakaokubaliwa.
Nchi zinazoshiriki Mkutano huo ni Angola, Afrika Kusini, Comoro, Eswatini, Mauritius, Msumbiji, Madagascar, Namibia, Visiwa vya Shelisheli, Zambia, Zimbabwe na Mwenyekiti Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
MWISHO.
0 comments:
Post a Comment