Musa Ndile
Na PETI SIYAME,Sumbawanga
Wanachama wa Chadema kutoka kata 19 zilizopo katika Manispaa ya Sumbawanga mkoani Rukwa wamemuomba Musa Ndile (35) aweke nia ya kugombea Ubunge Jimbo la Sumbawanga Mjini kwa tiketi ya chama hicho.
Njile ambaye ni mjasiriamali anaishi Jijini Dar es Salaam mwaka 2015 aliweka nia ya kugombea ubunge Jimbo la Sumbawanga Mjini kwa tiketi ya Chadema lakini katika kura za maoni kura hazikutosha alishika nafasi ya tatu.
Wakizungumza na wanahabari wanachama hao wameeleza kuwa hawako tayari kumchagua mgombea kwa utajiri wake wala kwa kupewa rushwa bali wanamtaka Ndile kwa kuwa ni mwadilifu na msikivu anachukia rushwa .
Judith Ulaya anasema anaamini kuwa hawezi kukisaliti chama kutokana na ukomavu na uvumilivu wake kisiasa
"Licha ya kushindwa katika kura za maoni 2015 Ndile alishirikiana bega kwa bega akimuunga mkono mkombea wa ubunge Jimbo la Sumbawanga Mjini kwa tiketi ya Chadema", alieleza.
Kauli hiyo iliungwa mkono na wanachama wengine akiwemo James Kafumu katika Kata ya Isesa na Grace Chiwala.
"Ndile ameonyesha ukomavu kwa kisiasa kwani hajakisaliti chama chetu kwa kujiunga na chama kingine cha siasa licha ya kubwagwa katika kura za maoni mwaka 2015.... Kwa niaba ya wazee wa Manispaa ya Sumbawanga tunamuomba popote alipo arudi nyumbani aweke nia ...tunauhitaji agombee ubunge katika Jimbo la Sumbawanga Mjini" alisisitiza Pascal Gerald kwa niaba ya wazee
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa njia ya simu Njile amekiri kuombwa na wanachama wenzake vijana kwa wazee kuweka nia ya kugombea ubunge katika Jimbo la Sumbawanga Mjini.
Hadi sasa wanachama watano wametangaza kujitosa katika kinyang'anyiro cha kugombea ubunge katika Jimbo la Sumbawanga Mjini kwa tiketi ya Chadema.
Wanachama hao ni pamoja na Sadrack Malila aliyegombea mwaka 2015 ,Dickson Mwanandenje,Pius Nguvumali Hosea Mtega na Richard Malisawa.
Mbunge wa Jimbo la Sumbawanga Mjini ni Aish Hilaly (CCM).
0 comments:
Post a Comment