Tuesday, 11 May 2021

Ushirika Kuja Na Suluhisho Ya Vifungashio

...

 


Chama Kikuu cha Ushirika Songea Namtumbo (SONAMCU LTD) Ruvuma kimesema tayari chama hicho kiko katika ujenzi wa Kiwanda cha vifungashio kwa lengo la kuhakikisha wakulima Mkoani Ruvuma wanaondokana na changamoto ya Vifungashio vya mazao ya mahindi, ufuta, soya na mbaazi.

Hayo yamesemwa na Meneja wa SONAMCU Juma Mwanga wakati akitoa maelezo kwa Mrajis wa Vyama vya Ushirika Dkt. Benson Ndiege alipotembelea kuona maendeleo ya mradi huo uliopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo Mei 10,2021 Mkoani Ruvuma.

Akitoa maelezo ya mradi Meneja huyo ameeleza kuwa licha ya Kiwanda hicho kuzalisha vifungashio kwa bei nafuu na upatikanaji rahisi wa vifungashio kwa wakazi wa Ruvuma na kuongeza mapato kwa wananchi mkoani hapo. Alisema Kiwanda hicho kinamilikiwa na wanachama wa SONAMCU kwa asilimia (100%) na kinatarajia kugharimu Shillingi 3, 983,889, 800 za Kitanzania. Akibainisha kuwa mradi huo ulianza mwaka 2020 na kukadiriwa kukamilika ifikapo 2022.

“Kwa sasa SONAMCU inapata bidhaa ya vifungashio kutoka Dar es salaam lakini tunatarajia kiwanda kitakapokamilika kitakuwa na uwezo wa kuzalisha vifungashio Millioni 10 kwa mwaka,” alisema Meneja

Aidha, Meneja alieleza kuwa hadi kufikia hatua hiyo ya  ujenzi kiwanda hicho kinajengwa kwa kutumia mapato ya ndani kwa asilimia (100%) mapato ambayo yanatokana na vyanzo mbalimbali vya Chama hicho. Aliongeza kuwa Chama kitatumia mkopo kutoka taasisi za fedha

Katibu Tawala Wilaya ya Namtumbo Aden Nchimbi katika ziara hiyo amesema Wilaya ya Namtumbo inatarajia kunufaika na mradi huo kutokana na ajira zitakazozalishwa na kiwanda hicho na kuchochea maendeleo ya Wananchi wa eneo hilo pamoja na Mkoa wa Ruvuma.

Kwa upande wake Mrajis Dkt. Ndiege amepongeza ujenzi wa Kiwanda hiko akibainisha kuwa soko la vifungashio hivyo ni kubwa kutokana na mazao mbalimbali yanayozalishwa na Vyama vya Ushirika ndani na nje ya Mkoa wa Ruvuma.

“Kutokana na uhitaji mkubwa wa vifungashio vya mazao ni matarajio yetu kuwa Vyama vya Ushirika vitakuwa wateja na wanunuzi wakubwa wa vifungashio hivyo na nipongeze Chama hiki kwa kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali za kuendeleza Viwanda nchini,” alisema Dkt. Ndiege  

Katika hatua nyingine, Chama Kikuu cha Ushirika SONAMCU kimeendesha mnada wa kwanza wa Ufuta katika mkoa wa Ruvuma Mei 10, 2021 katika eneo la soko la OTC Lilambo Ruvuma huu ukiwa ni mnada wa pili wa Ufuta kitaifa wakati mnada wa Kwanza tayari ulishafanyika Mkoani Songwe hivi karibuni.

Katika mnada huo Mrajis alipata fursa ya kueleza kuwa Mfumo wa Stakabadhi za Ghala unatoa faida kwa pande zote za muuzaji na mnunuzi. Akiongeza kuwa ukusanyaji mkubwa ni rahisi kutokana na wakulima kukusanya mazao yao kwa pamoja ghalani badala ya mnunuzi kutumia gharama kufuata mkulima mmoja mmoja katika maeneo tofauti. Akiongeza kuwa hii ni pamoja na udhibiti wa ubora unaosimamiwa kupitia Ushirika.

“Ruvuma ni kati ya mikoa ambayo imekuwa ikifanya vizuri katika Mfumo wa Stakabadhi za Ghala kutokana na kuuza mazao mbalimbali ikiwemo korosho, ufuta, soya na mbaazi ambapo mfanyabiashara na mkulima wote wanapata faida,” alisema Mrajis   

Mnada ambao Jumla ya wanunuzi tisa walishiriki ambapo bei ya juu ilikuwa ni shillingi 2,210 na bei ya chini ikiwa ni 1,750. Bei ambazo wakulima waliamua kuahirisha mnada huo ili kupata bei zenye tija zaidi zitakazowawezesha kurudisha gharama zao za uzalishaji. Chama Kikuu SONAMCU kitatangaza mnada mwingine wakati ukusanyaji wa Ufuta ukiendelea kwenye maghala mkoani hapo. 
  


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger