Monday 10 May 2021

SERIKALI INAHITAJI SHILINGI TRILIONI NANE KUSAMBAZA UMEME KATIKA VITONGOJI VYOTE

...

Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Mhandisi Leonard Masanja akifungua Mkutano wa Kwanza wa Mwaka baina ya REA na Wabia wa Maendeleo wanaofadhili miradi ya nishati uliofanyika tarehe 7,2021 jijini Dodoma.
Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Wakili Juliusi Kalolo,akizungumza wakati wa mkutano wa Kwanza wa Mwaka baina ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na Wabia wa Maendeleo wanaofadhili miradi ya nishati uliofanyika Mei 7,2021 jijini Dodoma.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Jones Olotu, akizungumza wakati wa mkutano wa Kwanza wa Mwaka baina ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na Wabia wa Maendeleo wanaofadhili miradi ya nishati uliofanyika Mei 7,2021 jijini Dodoma.

**********************

Na Jaina Msuya - REA

Serikali inahitaji zaidi ya Shilingi Trilioni Nane kwa ajili ya kusambaza miundombinu ya umeme katika vitongoji ambavyo havijafikiwa na nishati hiyo.

Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Wakili Julius Kalolo alisema hayo katika Mkutano wa Kwanza wa Mwaka kati ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na Wabia wa Maendeleo wanaofadhili miradi ya nishati kilichofanyika tarehe 7 Mei 2021.

Wakili Kalolo alisema kuwa kazi ya kusambaza miundombinu ya umeme katika vijiji vilivyobaki inaenda sambamba na kupeleka umeme katika vitongoji kupitia miradi ya ujazilizi.

"Vijiji vilivyobaki ni vichache hivyo kwa wakati huu pia tunaendelea na zoezi la kupunguza idadi ya vitongoji ambavyo havina umeme" alisema.

Akizungumzia lengo la kikao hicho, Wakili Kalolo alisema kuwa ni pamoja na REA kuwasilisha Mpango Kazi wa Mwaka ujao wa Fedha pamoja na Mpango wa Miaka Mitano wa REA kwa ajili ya kujadiliwa na Wabia wa Maendeleo kwa lengo la kutathmini utekelezaji wa mipango hiyo.

"Moja ya mambo tunayotarajia katika kikao hiki ni ahadi kutoka kwa wafadhili kuhusu utayari wao wa kusaidia katika baadhi ya maeneo. Ni muhimu tujenge hoja zinazokidhi vigezo vyao vya kupata ufadhili," alisema Wakili Kalolo.

Awali, akifungua Mkutano huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Leonard Masanja alisema kuwa utekelezaji wa miradi ya kusambaza umeme vijijini umeongeza fursa za uwekezaji katika maeneo ya vijijini. Alitoa wito kwa wananchi kutumia umeme kwa ajili ya shughuli za maendeleo ikiwa ni pamoja na kuanzisha biashara ndogo ndogo na za kati pamoja na viwanda.

"Umeme ni nyenzo muhimu kwa ajili ya maendeleo, ukiwa na umeme fursa nyingi za biashara zinafunguka," alisema.

Mhandisi Masanja alitoa wito kwa viongozi wa vijiji na mitaa kuwahamasisha wananchi kutoa maeneo yao kwa ajili ya kupitisha miundombinu ya kusambaza umeme pamoja na kutoa ushirikiano kwa kutunza na kulinda miundombinu hiyo.

"Nchi yetu imepiga hatua kubwa sana katika kusambaza umeme vijijini. Mwaka 2015 ni vijiji takribani 2,000 tu vilikuwa na umeme, lakini leo tunazungumzia vijiji 10,400 vyenye umeme kati ya vijiji 12,268 vya Tanzania Bara," alisema

Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini, Mhandisi Jones Olotu aliwataka wananchi kuchangamkia fursa ya kuunganishiwa umeme ili waweze kuanzisha miradi mbalimbali itakayowainua kiuchumi.

Mhandisi Olotu alisema katika baadhi ya maeneo mwitikio wa wananchi kuunganisha umeme bado upo chini na kuwataka kuunganisha umeme kwa bei nafuu ya Shilingi elfu 27.

Kwa wale wasioweza kumudu gharama za kutandaza nyaya katika nyumba zao aliwahamasisha kutumia kifaa maalum kijulikanacho kama Umeme Tayari ambacho ni mbadala wa _wiring_.

Akizungumza katika Mkutano huo, Mwenyekiti wa Wabia hao wa Maendeleo, Børjn Midthun aliipongeza REA kwa kazi nzuri ya kusambaza nishati vijijini na kuongeza kuwa imefungua fursa ya uwekezaji wa miradi ya nishati vijijini.

Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger