Askofu wa KKKT Dayosisi Kusini Mshariki ya Ziwa Victoria, Dkt. Emmanuel Joseph Makala akizungumza wakati akifungua mkutano wa halmashauri kuu ya dayosisi hiyo leo
Na Frank Mshana, Shinyanga
Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) limeshauriwa kupima maeneo yote yanayomilikiwa na Kanisa hilo na kupata hati za umiliki kwa lengo la kuepuka migogoro ya ardhi ambayo imekuwa ikijitokeza mara kwa mara baina ya Kanisa na baadhi ya watu wasio na hofu ya Mungu wanaotaka kupora maeneo ya Kanisa yaliyokaa muda mrefu bila kupimwa na kutambuliwa rasmi kuwa ni mali za kanisa.
Ushauri huo umetolewa na baadhi ya wajumbe wa Halmashauri kuu ya KKKT Dayosisi Kusini Mashariki ya Ziwa Victoria katika mkutano wa Halmashauri kuu ya Dayosisi hiyo uliofanyika Mei 14 na 15, mwaka huu katika viwanja vya Shule ya Sekondari Mwadui inayomilikiwa na KKKT Dayosisi Kusini Mashariki ya Ziwa Victoria.
Akizungumzia umuhimu wa Kanisa kupima maeneo na kutambua mipaka halisi ya maeneo Kamishna wa ardhi mkoa wa Shinyanga, Ezekieli Kitilya amesema yuko tayari kushiriki bega kwa bega kuhakikisha maeneo ya Kanisa yanapimwa na kupewa hati miliki lengo likiwa ni kuepuka migogoro ya ardhi inayosababisha maeneo mengi ya Makanisa kuporwa na watu wachache wasio na hofu ya Mungu.
Akizungumzia baadhi ya mifano ya maeneo ya Kanisa ambayo yamepata changamoto kama hiyo Mkuu wa Jimbo la Magharibi Kahama Mchungaji, Dkt. Daniel Mono amelitaja eneo la Bushushu ambalo linajengwa makao makuu ya Dayosisi kuwa ni mfano wa maeneo ya Kanisa la KKT yaliyokumbwa na changamoto ya kuvamiwa na kusababisha mgogoro uliowahi kufika Mahakamani huku akiunga mkono ushauri wa wajumbe wengine wa Halmashauri kuu juu ya upimaji wa maeneo yanayomiulikiwa na Kanisa.
Kwa upande wake, Askofu wa KKKT Dayosisi Kusini Mshariki ya Ziwa Victoria, Dkt. Emmanuel Joseph Makala ameunga mkono hoja hiyo na kuagiza mchakato wa kupima maeneo ya Kanisa uanze mara moja huku akiwataka waumini wa Kanisa la KKT katika Mikoa inayounda Dayosisi hiyo ambayo ni Shinyanga na Simiyu kutumia fursa ya uwepo wa Ofisi ya Kamishna wa ardhi Mkoani Shinyanga kupima maeneo yao ya makazi, biashara pamoja na mashamba ambapo Kamishna wa Ardhi, Ezekiel Kitilya ameahidi kutoa ushirikiano.
Mwisho viongozi pamoja na wajumbe wa Halmashauri kuu ya dayosisi wakaweka patano muda usiozidi mwaka mmoja kazi ya kuainisha, kupima na kuyatambua maeneo yote yanayomilikiwa na Kanisa iwe imefanyika.
Pamoja na agenda nyingine, mkutano ulikuwa na agenda ya Mkutano Mkuu wa tano wa Dayosisi ambao umepangwa kufanyika Juni 25 na 26, mwaka huu katika ukumbi wa Shule ya Sekondari Mwadui.
MATUKIO MBALIMBALI KATIKA PICHA
Askofu wa KKKT Dayosisi Kusini Mshariki ya Ziwa Victoria, Dkt. Emmanuel Joseph Makala akifungua mkutano huo
Mkuu wa Jimbo la Magharibi Kahama Mchungaji, Dkt. Daniel Mono akielezea mambo mbalimbali kwenye mkutano huo
Kamishna wa ardhi mkoa wa Shinyanga, Ezekieli Kitilya akielezea utayari wa ofisi yake katika kulisaidia kanisa hilo kupima maeneo yake ya ardhi inayoyamiliki
Mkutano ukiendelea
Baadhi ya wajumbe wakichangia hoja mbalimbali
Picha ya pamoja Wajumbe wa Halmashauri Kuu, Wenyevuti wa Kamati mbalimbali, Wakuu wa Majimbo, Viongozi mbalimbali,Askofu Msaidizi Mch. Yohana Ernest Nzelu na Askofu Emmanuel Joseph Makala baada ya kumalizika Mkutano
0 comments:
Post a Comment