Katibu Mkuu wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Hassan Abbasi amezitaka Kampuni za Ubashiri wa Michezo (Sports Betting) kuwa sehemu ya kuinua na kukuza michezo nchini.
Dkt. Abbasi ameyasema hayo Mei 05, 2021 Jijini Dar es Salaam katika kikao na Kampuni hizo ambapo amesema kuwa Michezo ya Kubashiri ( Sports Betting) inayo nafasi kubwa katika kuchangia maendeleo ya timu za Taifa hasa pale zinapokuwa katika mashindano.
“Lengo la Serikali kwa sasa ni kuwekeza kimkakati kwenye michezo, tuwe na mpango wa moja kwa moja wa kuzisaidia timu zetu za Taifa kifedha, mimi naamini tukishirikiana kwa karibu tunaweza kuleta mabadiliko chanya katika sekta ya michezo.” Alisema Dkt. Abbasi.
Katibu Mkuu Dkt.Abbasi amesisitiza kuwa changamoto zilizopo katika Kampuni hizo zitatafutiwa ufumbuzi kupitia vikao na njia mbalimbali baina ya Serikali na Kampuni hizo, ambapo amesisitiza ushirikiano kwa pande hizo mbili katika kusaidia nchi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama Cha Ubashiri wa Michezo Tanzania (TSBA) Jimmy Kenneth ameiomba Serikali kutatua baadhi ya changamoto ikiwemo uwepo kwa kampuni za ubashiri ambazo hazina usajili nchini ambazo zinaisababishia nchi kukosa mapato ambapo Dkt.Abbasi ameahidi kufanyia kazi suala hilo.
Naye Mwakilishi kutoka Biko Sports Goodhope Heaven alimshukuru Dkt. Abbasi kwa kuweza kukutana nao na kumshukuru kwa namna alivyoonesha moyo wa kusaidia Sekta ya Michezo nchini pamoja na kuwa mstari wa mbele katika kutatua changamoto zao.
Wadau hao kwa pamoja wameonesha utayari wa kuzisaidia timu za Taifa huku wakiiomba Serikali kuweka msisitizo wa mazingira rafiki ya ulipaji kodi.
0 comments:
Post a Comment