Na Faraja Mpina, WMTH, Dodoma
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Zainab Chaula amefungua mafunzo ya kuwajengea uwezo wasichana na wanawake ili waweze kushiriki kikamilifu katika masuala ya ubunifu katika sekta mbalimbali ambapo kwa namna moja ama nyingine watatumia TEHAMA katika kufanya tafiti zao na kutafuta masoko ya kuuza na kununua bidhaa zao.
Akifungua mafunzo hayo yaliyofanyika jijini Dodoma Dkt. Chaula ametoa rai kwa waandaaji wa mafunzo hayo kuongeza wigo wa washiriki hasa wanaohusika na kutoa maamuzi kwa kuwa Serikali imejipanga kutambua, kuwezesha na kuendeleza ubunifu na teknolojia zinazozalishwa nchini ambapo hadi sasa ushiriki wa watoto wa kike na wanawake bado ni mdogo sana.
“Ubunifu ni namna mtu anakuja na jambo lake jipya, analiunda mwenyewe, analitengeneza mwenyewe, analisimamia mwenyewe kulingana na fikra zake ndio maana hapa leo tupo na Ndoto Hub kila mtu anaishi kulingana na fikra na ndoto zake, anatamani afikie sehemu fulani na kuwashawishi wengine ili nao wapate ndoto kupitia wengine”, alizungumza Dkt. Chaula
Ameongeza kuwa ni muhimu dhana nzima ya ubunifu kueleweka kwa jamii sambamba na kuangazia madhara ya kutohusisha mwanamke na mtoto wa kike katika masuala ya ubunifu na madhara ya kutokuendeleza ubunifu ulioletwa na wabunifu katika maeneo mbalimbali ya kisekta ili Serikali iweze kufanyia kazi maeneo ambayo yataainishwa.
Akizungumza katika mafunzo hayo Mbunge wa viti maalum CCM kutoka katika kundi la Asasi za Kiraia Tanzania Bara Mhe. Neema Lugangira amesema kuwa wapo katika mafunzo hayo kujadili kwa pamoja na kuona namna ambayo mwanawake na mtoto wa kike wanaweza kushiriki katika masuala ya ubunifu na teknolojia kwa kuziangazia changamoto zinazowakwamisha na kuzitafutia ufumbuzi.
Naye Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) Justina Mashiba amesema kuwa wao kana taasisi ya umma wana jukumu la kuhakikisha inawasaidia na kuwawezesha watoto wa kike katika TEHAMA na kuhakikisha hawapo nyuma katika masuala ya ubunifu katika TEHAMA.
Kwa upande wa Mkurugenzi Mkuu wa Ndoto Hub na Shule Direct Faraja Kotta Nyalandu amesema kuwa mafunzo hayo ni moja ya majukwaa ya kuwawezesha wanawake na wasichana kutafuta fursa za biashara na kufanya ujasiriamali kupitia TEHAMA.
Mafunzo hayo yamefanyika chini ya uratibu wa Capital Space, Ndoto Hub, Tanzania Community Network Alliance na wadau mbalimbali wakiwemo HDIF, Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) na Segal Family Foundation kwa lengo la kutengeneza mazingira rafiki ya ubunifu kwa wanawake na watoto wa kike ili waweze kushiriki kikamilifu katika masuala ya ubunifu na teknolojia.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari
0 comments:
Post a Comment