Na Abby Nkungu, Singida
SERIKALI imeombwa kuangalia uwezekano wa kupunguza kodi ya vifaa mbalimbali vinavyoingizwa nchini na wawekezaji wa ndani kwa ajili ya kutaka kuanzisha miradi inayolenga kuboresha huduma za jamii.
Rai hiyo imetolewa na Mmiliki wa Katala High School iliyopo mjini Kiomboi Wilaya ya Iramba mkoani Singida, Jumbe Katala wakati wa hafla maalum kwa ajili ya kutambulisha shule hiyo kwa umma.
Alisema kuwa licha ya Watanzania wengi waliopo nje ya nchi kutaka kuunga mkono juhudi za Serikali za kuboresha huduma za kijamii kwa kuwekeza miradi mbalimbali nyumbani, hatua hiyo imekuwa ikikwamishwa na utitiri wa kodi kwa vifaa wanavyoingiza kwa ajili ya shughuli husika.
Alitolea mfano wa moja ya shehena zake za mizigo iliyokuwa imebeba vifaa mbalimbali ambavyo alikuwa ameagiza kutoka nje ya nchi kwa ajili ya matumizi ya shule hiyo ambayo anadai ilitozwa kodi kubwa.
"Ushauri wangu kwa Serikali, Wawekezaji wa ndani wapewe upendeleo wa kutozwa kodi nafuu wanapoingiza vifaa mbalimbali kwa ajili ya utekelezaji wa miradi yao inayohusu huduma za kijamii" alisema na kuongeza;
Hali ilivyo hivi sasa, kodi iko juu sana kiasi cha kumvunja moyo mwekezaji yeyote; hasa sisi tunaoishi nje ya nchi tukija na vifaa tunatozwa kodi asilimia 100 ya gharama hali inayoweza kusababisha baadhi yetu kukata tamaa ya kuendelea na miradi tunayokusudia kuanzisha.
Alisema kuwa wale ambao walipewa fursa ya kufutiwa au kupunguziwa kodi wakavunja uaminifu, wanaweza kushughulikiwa kama wahalifu wengine na kwamba hiyo isiwe sababu ya kuwanyima unafuu wa kodi Wawekezaji wengine walio waaminifu na wenye nia njema ya kuisadia Serikali katika kuleta maendeleo ya nchi.
"Tunapoamua kuja kuwekeza nchini tunakusudia, mbali na kuiunga mkono Serikali yetu katika suala la maendeleo, lakini pia tunaleta fursa za ajira kwa wananchi wetu; hivyo kuipunguzia Serikali mzigo wa watu wasio na ajira. Kodi kubwa imekuwa ni changamoto kwetu" alisema na kufafanua;
Sisi tunaoishi nje ya nchi tunaona ni bora kununua vifaa huko tulipo ili kukwepa kudhulumiwa na ndugu zetu iwapo utadiriki kutuma fedha kwa ajili ya ununuzi wa vifaa hivyo hapa nchini. Kodi inapokuwa mara mbili ya gharama ya vifaa ulivyonunua, hakika inakatisha sana tamaa"
Alisema kuwa wazo la kujenga shule hiyo mwaka 2015 lilikuja baada ya kuona kumekuwa na idadi kubwa ya shule za Sekondari zenye kidato cha nne wakati hakuna hata shule moja yenye kidato cha tano wilayani humo; hivyo kukamilika kwa ujenzi wa shule hii kutaziba pengo lililopo.
Alisema shule hiyo ambayo itagharimu zaidi ya Sh bilioni 1.5 itakapokamika na kuchukua wanafunzi 500 wa kidato cha Tano na Sita, itaanza rasmi July mwaka huu ambapo kwa kuanzia wanafunzi 100 tu wa kidato cha tano watadahiliwa.
"Nia yetu ni kuwa Kituo cha Umahiri wa kitaaluma ambapo wanafunzi watakaohitimu masomo yao hapa watakuwa wameiva barabara ili kuweza kuchangia kwenye soko la Viwanda. Baada ya kukamilisha ujenzi wa A level tuna mpango wa kujenga Chuo Kikuu kisha shule ya Sekondari kidato cha kwanza hadi cha nne huko kijiji cha Ruruma wilayani humu" alieleza.
Hata hivyo, baadhi ya wananchi wa eneo hilo licha ya kumpongeza Mwekezaji huyo kwa kuona umuhimu wa kuanzisha shule ya kidato cha tano na sita, wamekuwa na maoni tofauti juu ya suala la kodi.
Wengi walisema kuwa suala la kodi halina mbadala kutokana na ukweli kwamba hiyo ni moja ya njia kuu za kuiingizia mapato Serikali ili iweze kutekeleza kwa ufanisi majukumu yake mbalimbali huku baadhi wakiunga mkono hoja ya kupunguziwa kodi wawekezaji wa sekta ya elimu na nyingine zinazohusu huduma za jamii.
0 comments:
Post a Comment