Na. OWM, Kigoma.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu), Mhe. Jenista Mhagama (Mb), ameitaja mikoa 11 ambayo ilianzisha mabaraza ya Biashara na hadi sasa yako hai na kubainisha kuwa mikoa mingine ilitekeleza agizo la kuanzisha mabaraza hayo tu lakini utendaji wa Mabaraza hayo umekuwa siyo endelevu.
Waziri Mhagama ameitaja Mikoa hiyo 11 ambayo Mabaraza yake yako hai hadi sasa kuwa ni Dodoma, Kigoma, Tanga, Geita, Morogoro, shinyanga, Dar es Salaam, Pwani, Iringa, Songwe na Mbeya. Aidha, Mhagama amebainisha kuwa Mikoa mingine ambayo mabaraza yake hayafanyi vikao inakiuka Waraka wa Rais Na. 1 wa mwaka 2001 unaosisitiza kuanzishwa kwa mabaraza hayo na utendaji wake kuwa endelevu.
Akiongea wakati wa kufuatilia utekelezaji wa shughuli za Baraza la Taifa la Biashara mkoani Kigoma, Waziri Mhagama alifafanua kuwa Dhumuni kuu la kuanzisha mabaraza ya biashara hususani katika ngazi ya wilaya na mikoa ni kuweka mfumo rasmi wa kuwakutanisha viongozi wakuu wa Serikali na Sekta Binafsi katika kila ngazi ya utawala, kujadiliana jinsi ya kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini kwa ajili ya kukuza sekta binafsi ambayo ndio muhimili muhimu wa kukuza uchumi wa nchi.
“Hatuwezi kuwa tunamshuhudia Mhe. Rais wa awamu ya tano Dkt. John Pombe Magufuli anaitisha vikao vya Baraza la Taifa la Biashara katika ngazi ya Taifa lakini katika ngazi ya mkoa na wilaya hamtekelezi maagizo hayo, lazima mabaraza yakutane ili kutatua kero za wafanyabiashara na wawekezaji katika ngazi ya mkoa na wilaya, lakini pia itasaidia kuibua fursa za uwekezaji na kuzinadi fursa hizo, na sisi tumeamua kukagua mkoa mmoja baada ya mwingine ili kupunguza kero za wafanya biashara na wawekezaji” Amesema Mhagama
Wakiongea kwa nyakati tofauti wakati Waziri Mhagama alipokutana na Wajumbe wa Baraza la Mkoa la Biashara, Mkuu wa mkoa wa Kigoma, Brigedia Jenerali Mstaafu, Emmanuel Maganga , Mkuu wa wilaya ya Kigoma, Samson Anga na Katibu Tawala wa Mkoa huo, Rashid Mchata, walieleza kuwa kupitia Mradi wa Kuboresha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji (LIC), wameweza kuimarisha mfumo wa majadiliano kati ya serikali na sekta binafsi kupitia Mabaraza ya Biashara ya Mikoa na Wilaya.
Naye Mratibu wa Mradi huo, Andrew Mhina alibainisha kuwa Mradi huo unalenga kuhakikisha kuwa unaboresha mazingira ya Biashara na uwekezaji nchini tayari kwa kushirikiana Baraza la Taifa la Biashara wameandaa mwongozo wa Majadiliano Kati ya Serikali na Sekta Binafsi ngazi ya Mkoa na Wilaya ili kuyajengea uwezo Mabaraza ya Mikoa yaweze kuwa endelevu na yenye ufanisi.
Baraza la Taifa la Biashara lilianzishwa kwa Waraka wa Rais Na. 1 wa mwaka 2001 na kuchapishwa kwenye Gazeti la Serikali Na. 39 la tarehe 28 Septemba 2001. Baraza hilo ni jukwaa la majadiliano kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi, na lengo kuu la Baraza ni kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji kwa njia ya majadiliano kati ya sekta ya umma na sekta binafsi.Aidha Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Biashara ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
0 comments:
Post a Comment