Sunday, 30 December 2018

SERIKALI YATOA UFAFANUZI KUHUSU SAKATA LA MWANANCHI KUKAMATWA AKISAFIRISHA VITANDA VIWILI

...
Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) umepokea taarifa kupitia mitandao ya kijamii na wadau mbalimbali zinazohusisha namna Afisa Misitu wa Wilaya ya Korogwe alivyokuwa akitekeleza majukumu ya kusimamia Sheria ya Misitu Na. 14 ya Mwaka 2002 pamoja na Kanuni zake za Mwaka 2004.

 Afisa huyo alikuwa akitekeleza majukumu hayo kwa mujibu wa kifungu cha 93 (Powers of officers with respect to offences) inayompa mamlaka Afisa Misitu au Afisa wa Jeshi la Polisi kukagua, kukamata na kuzuia mazao yanayodhaniwa kupatikana kinyume na sheria.

Kufuatia taarifa hizo, uongozi wa TFS umefanya uchunguzi wa haraka na kubaini kuwa abiria mmoja alikuwa akisafirisha vitanda viwili (2) vipya kwa basi. Vitanda hivyo vililipiwa ushuru wa Serikali kupitia mfumo wa Kielektroniki wa Malipo Serikalini (GePG) na kupewa stakabadhi halali ya tarehe 26 Disemba, 2018 katika kituo cha Mkata, Handeni Mkoani Tanga.

Katika kutekeleza majukumu yake, Afisa wetu alimtaka abiria huyo kuonesha Hati ya Kusafirishia (Transit Pass) bidhaa hizo kwa mujibu wa Kanuni ya 13(4) ambayo inakataza mwenye chombo chochote cha usafiri kusafirisha mazao ya misitu ambayo hayana hati ya usafirishaji ambapo abiria huyo hakuwa nayo. 

Hata hivyo, Afisa wetu alishindwa kutafsiri masharti ya kifungu hiki na mahitaji ya utoaji wa Hati ya Usafirishaji kwani kama msafirishaji binafsi kwa matumizi ya nyumbani asingeweza kukidhi vigezo vya kuwa na hati hiyo. 

Hati ya Usafirishaji huhitaji msafirishaji kuonesha usajili, leseni ya biashara, utambulisho wa mlipa kodi na namba ya usajili wa chombo kinachotumika kusafirisha mazao hayo pamoja na kuonesha vituo atakavyopaswa kukaguliwa.

Kufutia tukio hilo, Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania unamwomba radhi abiria huyo na umma wa watanzania kwa tukio hilo na usumbufu uliojitokeza. Wakala unaendelea kufuatilia suala hili, na utahakikisha kuwa tukio kama hili halijirudii tena.

 Aidha, hatua za kinidhamu zitachukuliwa kwa mujibu wa Kanuni za utumishi wa umma dhidi ya mtumishi aliyehusika na utoaji wa lugha isiyo na staha wakati akitekeleza sheria ya misitu ambapo alitegemewa kutoa elimu stahiki kwa umma. Hivyo, TFS inapenda kufafanua mambo yafuatayo:- 2

1. Kwamba ikiwa mwananchi yeyote amenunua samani mpya kutoka kwa watengenezaji au wauzaji mahali popote kuhakikisha anapatiwa risiti halali kwa malipo aliyofanya. Hivyo, mmiliki wa samani mpya kwa matumizi binafsi halazimiki kuwa na Hati ya Usafirishaji anaposafirisha toka eneo moja kwenda jingine isipokuwa awe tayari kuonesha uthibitisho wa nyaraka za malipo halali ya samani hizo kwa ukaguzi pale itakapohitajika.

2. Mwananchi yeyote anayesafirisha samani zilizotumika kutoka eneo moja hadi jingine halazimiki kuwa hati za malipo wala kuwa na hati ya kusafirishia samani hizo.

3. Serikali itaendelea kufanya mapitio ya Sheria ya Misitu na Kanuni zake ili kuepuka mkanganyiko wowote wa tafsiri ya sheria unaoweza kujitokeza na kuondoa usumbufu kwa wananchi.

Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania unapenda kutoa rai kwa wananchi wote kuendelea kuzingatia Sheria za uhifadhi wa misitu. Aidha, Wakala hauna nia ya kuzuia utengenezaji, usafirishaji na matumizi ya samani za mbao mahali popote nchini ilimradi tu upatikanaji wa malighafi zake uwe umefuata utaratibu. Lengo ni kuhakikisha kuwa rasilimali za misitu zinatunzwa na kutumika kwa njia endelevu kwa maendeleo ya Taifa. Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania utaendelea kutoa elimu kwa umma pamoja na watumishi wake kuhusu taratibu za uvunaji, usafirishaji na biashara ya mazao ya misitu nchini kupitia njia mbalimbali na kuhakikisha huduma bora kwa wananchi.

IMETOLEWA NA
KITENGO CHA HABARI NA MAWASILIANO KWA UMMA
WAKALA WA HUDUMA ZA MISITU TANZANIA (TFS)
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger