Saturday, 29 December 2018

DED,WATUMISHI 12 MATATANI KWA KUTAFUNA BILIONI 2.9

...

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Ulanga mkoani Morogoro, Yusufu Semguruka na watumishi 12 wanadaiwa kutafuna zaidi ya Sh bilioni 2.9 za Serikali.

Kutokana na hali hiyo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo, ameelekeza watumishi hao wavuliwe madaraka na mamlaka za nidhamu na vyombo vya dola vifanye uchunguzi.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa jana, Jafo, alisema ofisi yake ilifanya uchunguzi maalumu kwa halmashauri 12 ikiwamo Ulanga.

Alisema malalamiko yalikuwa mengi kwa Ulanga kutoka kwa wananchi na Mbunge wa jimbo hilo, Goodluck Mlinga.

Alisema matokeo ya uchunguzi huo kwa halmashauri hiyo yamebaini matumizi mabaya ya fedha za Serikali zinazofikia Sh 2,980,172,763.60 na watumishi hao wasio waadilifu walikiuka taratibu za fedha, walihujumu na kufanya ununuzi hewa.

“Halmashauri imekuwa ikifanya udanganyifu katika taarifa za miradi ya maendeleo, kufanya manunuzi hewa, kutumia fedha tofauti na makusudio yaliyokusudiwa na udhibiti mbovu wa mapato ya Serikali,” alisema.

Aliwataja watumishi hao kuwa ni Semguruka, Mweka Hazina, Rajabu Siriwa, aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi katika halmashauri hiyo, David Kaijage, wahasibu Stanley Nyange, Isaack Salum, Johnson Mwanyombole na Saleh Mbogoso.

Aliwataja wengine kuwa ni wataalamu wa mifumo ya tehama katika halmashauri hiyo, Yasin Galahenga na Mohamed Said, Ofisa Mnunuzi, Willy Ndabila, Mhasibu wa Hospitali ya Wilaya ya Ulanga, Goodluck Mbata, Mganga wa Wilaya, Dk. Abdallah Risasi na Mfamasia wa Wilaya, Jackson Nyabusani.

JINSI WALIVYOTAFUNA FEDHA

Jafo alisema Semguruka alishindwa kusimamia sheria ya fedha za Serikali za Mitaa katika kudhibiti na kuweka mifumo ya kuhakikisha ziko salama kuanzia makusanyo hadi manunuzi.

“Hii ni pamoja na kushindwa kumsimamia mweka hazina wa halmashauri katika kuyatekeleza majukumu yake na hivyo kuisababishia hasara Serikali ya shilingi 2,980,172,763.60,” alisema.

Kwa upande wa Siriwa, alisema alichangia kuhujumu mapato ya halmashauri kwa kuweka utaratibu uliosababishia hasara.

“Kuidhinisha malipo ya shilingi 225,586,400 nje ya bajeti bila idhini ya ofisi ya Tamisemi, marekebisho ya bajeti hii yalihusisha posho za safari ya mkurugenzi shilingi 192,000,000. Kukusanya na kutopeleka benki shilingi 760,686,732.43.

“Kuandaa taarifa zenye udanganyifu kwa utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayotumia fedha za makusanyo ya ndani. Halmashauri inaripoti kupeleka shilingi 301,442,686 wakati uhalisia wamepeleka shilingi 113,406,106,34,” alisema.

Pia alisema amefanya udanganyifu katika fedha za mfuko wa vijana na akina mama baada ya halmashauri kuripoti kupeleka Sh 120,000,000 wakati uhalisia wakiwa wamepeleka Sh 31,500,000 kwa mwaka wa fedha wa 2017/2018.

“Kukusanya fedha na kuzihujumu, mweka hazina ndiye aliyemjulisha Kaijage mapokezi ya shilingi 470,000,000 lakini mara tu walipozipokea walifanya hujuma ya kuzilipa fedha hizo kwa kampuni iliyowalipa,” alisema.

Kuhusu Kaijage, alisema wakati akikaimu nafasi hiyo Februari mosi hadi Februari 8, mwaka huu alihusika kuihujumu halmashauri kwa mapato ya Sh 470,000,000 yaliyopokelewa kutoka Kiwanda cha Kilombero Valley Teak na kuzirejesha kwa mlipaji siku hiyo hiyo waliyopokea.

“Pia alisaini hati ya malipo kumlipa Bahari Pharmacy kwa siku ambayo hakuwa Kaimu Mkurugenzi na Mkurugenzi alikuwepo,” alisema.

Kwa upande wa wahasibu, Nyange na Salum wao wameihujumu halmashauri kwa kutumia akaunti binafsi kupokea fedha za makusanyo pamoja na kuchukua fedha kutoka vituo vya makusanyo na kutozipeleka benki.

Alisema kwa upande wa Galahenga na Said, wao walishirikiana na wahasibu kurekebisha ankara na kufuta madeni bila idhini ya mkurugenzi.

“Hawa wameihujumu mapato ya halmashauri kwa kufanya marekebisho ya ankara za wateja bila idhini ya mkurugenzi wala maombi ya wateja shilingi 79,926,747, yaani wao ndio wanaomba na wao ndio wanaidhinisha marekebisho,” alisema.

Jafo alisema Ndabila alihusika katika ununuzi hewa wa dawa zenye thamani ya Sh 73,212,909.40 pamoja na kulipa fedha zaidi ya Sh 146,425,818.

Kuhusu Mbata, alisema aliandaa malipo na kusainisha mara mbili kwa watu tofauti huku akijua kufanya hivyo ni kuandaa malipo mara mbili kwa hitaji moja.

Pia alisema Dk. Risasi na Nyabusani walifanya njama ya kununua dawa ambazo halmashauri hawakuzipokea lakini ililipa fedha zaidi ya zile za mkataba wa ununuzi.

“Halmashauri ililipa shilingi 146,425,818 badala ya Sh 73,212,909.40,” alisema.

AAGIZA WAVULIWE VYEO

Jafo alitoa maelekezo wakuu wa vitengo waliohusika Galahanga, Kaijage na Ndabila ambaye amehamishiwa Itilima, Siriwa aliyehamishiwa Gairo wavuliwe madaraka.

Pia watumishi waliohamishwa wakiwa na makosa warejeshwe Ulanga ili kuiwezesha halmashauri na vyombo vya dola kufanya kazi yake.

“Wahasibu waliohusika kuhujumu mapato waondolewe majukumu yao ili kupisha halmashauri na vyombo vya dola kufanya kazi yake. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro ieleze ni kwanini hawakuchukua stahiki zenye tija,” alisema.

MLINGA APONGEZA

Akizungumza kwa njia ya simu na gazeti hili, Mlinga, alifurahia uamuzi huo akidai watumishi hao walikuwa wakitafuna fedha za Serikali bila woga wowote.

Na Ramadhan Hassan-Dodoma
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger